MLANGO WA KIZAZI

MLANGO WA KIZAZI NI NINI?

Mlango wa kizazi (cervix) ni kiungo cha mwili kinachopatikana kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke. Ni sehemu ya mji wa mimba (Uterus) inayotokezea kwenye uke (tupu) wa mwanamke. Tazama picha ifuatayo

SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI?

Ni mabadiliko hasi (yasiyo ya kawaida) ya chembechembe hai zilizopo kwenye Mlango wa kizazi. Mara nyingi saratani hii ikiwa inaanza haionyeshi dalili yoyote hivyo mgonjwa hawezi kuchukua hatua yoyote kukabiliana na tatizo hili kwa wakati huu.

 Kwa kiasi kikubwa saratani hii husababishwa na maambukizi ya mda mrefu (persistence infection) ya virusi viitwavyo Human papilloma, ambavyo huenezwa kwa njia ya kujamiiana. Kawaida mwili una uwezo wa hudhibiti maambukizi haya yaingiapo mwilini, lakini yasipodhibitiwa kikamilifu na kuwepo mwilini kwa mda mrefu husababisha ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.

MAMBO MENGINE YANAYOCHANGIA KUPATA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI

  • Kufanya ngono zembe
  • Kuwa na wapenzi wengi
  • Kukoma siku katika umri mkubwa
  • Utumiaji mafuta mengi katika chakula.
  • Kutokufanya mazoezi ya mara kwa mara.
  • Unene kupita kiasi
  • Uvutaji sigara.
  • Utumiaji wa pombe kupita kiasi.
  • Historia ya saratani ya matiti katika familia.

DALILI ZA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI

Dalili za ugonjwa huu huanza kujitokeza baada ya tatizo kuanza kukomaa, zifuatazo ni baadhi ya dalili

  • Kutokwa na maji maji yenye harufu ukeni
  • Kutokwa damu baada ya kujamiiana
  • Kutokwa damu kusiko kwa kawaida (siyo damu ya hedhi)
  • Kuumwa mgongo na kiuno
  • Kuumwa miguu
  • Kizunguzungu na kuishiwa nguvu

NINI KIFANYIKE?

Saratani ya mlango wa kizazi inazuilika au kutibika kabisa endapo itagundulika ikiwa kwenye hatua za awali.

Hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya yako kwa kadiri utakavyoshauriwa na wataalam wa afya

Wanawake wote walio na umri kuanzia miaka 30 na kuendelea wanatakiwa kufanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.

Kumbuka: Wakati wa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi ni sasa usisubiri hadi uone dalili, fika kituo cha huduma za afya kwa ushauri/mwongozo Zaidi,