Maadhimisho ya siku ya saratani duniani

      Comments Off on

Maadhimisho ya siku ya saratani duniani

Katika kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuhimiza jamii kuchukua hatua madhubuti za kujikinga dhidi ya saratani na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Diwani msemo leo Februari 4, 2026 alipowasilisha hotuba ya waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani katika katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Dkt. Msemo amesema kuwa ili kuthibiti magonjwa yasioambukiza, watanzania wanatakiwa kubadilisha mtindo wa maisha ili kuimarisha afya ikiwemo kufanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 mara tano kwa wiki, kupunguza matumizi ya vilevi na kuacha kabisa matumizi ya tumbaku.

Aidha, Dkt. Msemo amesema Serikali inaendelea kuhimiza wananchi kujiunga na mfumo wa bima ya afya kwa wote, ili kuwezesha uchunguzi na matibabu ya mapema kabla ugonjwa haujafikia hatua hatarishi

Ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa afya, viongozi wa dini, taasisi za kijamii na vyombo vya habari umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kufikisha elimu sahihi kwa jamii.

Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani yanatumika kama wito wa pamoja kwa Watanzania wote kuendelea kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya saratani, kwa kubadili mtindo wa maisha, kuhamasishana kufanya uchunguzi wa mapema, na kuungana kwa pamoja kudhibiti saratani na magonjwa mengine yasiyoambukiza kwa mustakabali wa taifa lenye afya bora.