“Wauguzi wanatakiwa kuiga falsafa za Florence Nightingale” hayo ameyasema leo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Diwani Msemo katika maadhimisho ya siku ya wauguzi ngazi ya tawi la Ocean Road yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi hiyo.
Dkt. Msemo amewataka wauguzi kufanya kazi kama Florence Nightingale alivyokuwa akifanya ikiwemo kuwa na moyo wa huruma kwa wagonjwa.
Pamoja na hayo Dkt. Msemo ametoa nyongeza ya zawadi ya Mkurugenzi ya shilingi laki moja kwa Kila mfanyakazi bora waliopata zawadi katika maadhimisho hayo.
Vile vile ametoa ahadi ya kutatua changamoto zinazowakumba wauguzi kadiri Taasisi inavyokuwa na uwezo wa kutatua changamoto hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa uuguzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Bi. Mary Haule amesema muuguzi anatakiwa kutoa huduma za uuguzi kwa uadilifu wa hali ya juu.
Bi. Haule amekumbusha kuwa uuguzi ni moyo wa Taasisi na ndio sura ya Taasisi na wauguzi wanatakiwa kuhakikisha wanalinda sura ya Taasisi.
Vile vile Mwenyekiti wa TANNA tawi la Taasisi ya Saratani Ocean Road Bi. Herrieth Mbwana amesema tarehe 12 Mei Kila mwaka ndio maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani, na tarehe 23 mei ndio kilele Cha maadhimisho ya kudumisha muasisi na muanzilishi wa uuguzi Duniani Bi. Florence Nightingale.