Kambi ya uchunguzi wa saratani ya kizazi yaanza mkoani Tanga, Wanawake 1000 kuchunguzwa

      Comments Off on

Kambi ya uchunguzi wa saratani ya kizazi yaanza mkoani Tanga, Wanawake 1000 kuchunguzwa

Kambi maalum ya kampeni ya uchunguzi na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa Mkoa wa Tanga, imeanza rasmi leo Januari 28, 2021 ikitarajiwa kukamilika Januari 30, 2021, Wanawake wapatao 1,000 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi na wataalamu mabingwa wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).


Mabingwa hao wa ORCI wamepiga kambi hiyo wakishirikiana na Wataalamu wa  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, ambapo awali walianza kwa kuwapa mafunzo wahudumu wa afya katika kufanya   uchunguzi wa awali saratani ya mlango wa kizazi na matibabu.
“Tunawajengea uwezo watoa huduma Mkoa wa Tanga, Halmashauri na Wilaya zote za mkoa huu, washiriki waliohudhuria mafunzo haya ni zaidi ya 25, tunawakaribisha wakazi wa Tanga kutumia fursa hii ambapo tutakuwa hapa kwa ajili ya kuwahudumia,” amebainisha Dk. Kahesa

Ameongeza “Saratani ya kizazi inashika namba moja kwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudumiwa Ocean Road, Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa 10 ambako watu wameathirika na saratani hii, kwa hiyo program hii itasaidia kuibua wale wenye matatizo mapema, watapata matibabu mapema na hivyo tutaweza kujenga afya kwa kina mama

Wananchi wakisoma vipeperushi vya elimu kuhusu jinsi ya kutambua saratani ya mlango wa kizazi pamoja na saratani ya matiti walivyogawiwa

Amesema ingawa walengwa wakubwa wa kampeni hiyo ni wanawake, hata hivyo wanaume hawajaachwa nyuma na kwamba wale watakaofika hospitalini hapo watapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya tezidume, wasisite kujitokeza.
Akizungumza, Mkazi wa Tanga Mjini Jafari Ali amepongeza ushirikiano huo wa wataalamu wa Ocean Road na wenzao wa Mkoa wa Tanga kwa kufanya kampeni hiyo kwani imemuwezesha naye kupata fursa ya kufanya uchunguzi wa saratani ya tezidume.
“Niliona matangazo yaliyobandikwa, nikaamua kufika, nimepata vipimo wala hakuna tabu, nimechunguzwa kwa kipimo cha damu, leo tarehe 28 ni siku ya kwanza, 29 na 30 wataalamu watakuwa hapa Bombo, wanaume wenzangu wajitokeze na wanawake pia wafike kuchunguzwa saratani ya kizazi,” ametoa rai

Mkazi wa Wilaya ya Mkinga, Asia Hussein Ngoma amewasihi wakazi wenzake wa Tanga kuchangamkia fursa hiyo ya huduma ya uchunguzi na matibabu ya awali kwa saratani ya kizazi inayotolewa na wataalamu hao.
“Kule ninapoishi mimi ni kijijini, nilisikia matangazo redioni, nikafunga safari kuja hapa, nimekuonwa na madaktari, wamenichukua vipimo vizuri, wamenihudumia vizuri, nawasihi na wenzangu waje, waonwe na wataalamu hawa wenye lugha nzuri, huduma nzuri, wahudumiwe, wafarijike,” ametoa rai