Timu ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi waingia nchini Comoro kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan

      Comments Off on

Timu ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi waingia nchini Comoro kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan

Timu ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road inatarajia kuelekea Comoro kwaajili ya kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kupeleka madaktari hao katika Hospitali tofauti visiwani humo ili kuweza kuweka kambi maalum ya msaada wa huduma za kiuchunguzi na kimatibabu za Saratani.

Dkt. Diwani Msemo ambae ni mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road amesisitiza kuwa Taasisi ina wataalam wa kutosha ambao ni mabingwa bobezi kwenye upande wa Saratani hivyo wana uhakika wa huduma watakazokwenda kuzitoa huko hazina tofauti hata kidogo na zile zinazotolewa katika makao makuu ya Taasisi hiyo posta jijini Dar es Salaam.

Aidha Dkt. Msemo amewataka wananchi wa mji wa Anjouan kujitokeza kwa wingi katika kambi hiyo kwani huduma zitakazotolewa ni zenye ubora wa kimataifa na zitatolewa bila malipo yoyote.

Dkt. Msemo amezitaja Saratani zitakazofanyiwa uchunguzi kuwa ni zile za Matiti pamoja na Mlango wa kizazi kwa wakina mama, huku wakina baba wakifanyiwa uchunguzi na matibabu ya Saratani ya Tezi Dume.

Katika hatua nyingine, Dkt. Msemo amewatoa wasiwasi wakina baba kwa kuwajulisha kuwa uchunguzi wa Saratani kwa sasa hufanywa kwa njia rahisi mno ambapo inatolewa Damu kidogo kwenye kidole kama vinavyofanyika vipimo vya maleria kisha baada ya dakika Tano tu
Mtu anapata majibu yake, hivyo amesisitiza wakina baba kujitokeza kwa wingi katika Hospitali ya Howo ili kupata huduma hiyo.

Kambi hiyo maalum ya kimatibabu itafanyika kuanzia tarehe 05-12/10/2025, katika mji wa Anjouan unaopatikana Kisiwani Comoro.