ZIARA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII.
Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti Mhe. Stanslaus Nyongo ilifanya ziara tarehe 15/03/2021 kutembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Taasisi zilizoidhinishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan mradi wa ununuzi wa Mashine ya kisasa ya teknolojia ya nuclear medicine ya kupima saratani mwilini “Positron Emission Tomography Computerized Tomography scan (PET/CT scan)”.
Cyclotron
Ziara ya kamati hiyo ilianza kwa waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Nyongo pamoja na Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Dkt Dorothy Gwajima aliyeambatana na naibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt Godwin Mollel kukaribishwa katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, ambapo baada ya Risala ya Mwenyekiti wa Kamati na Utambulisho wa Washiriki, iliwasilishwa Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi na Mradi wa PET/CT Scan na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Mkurugenzi Mtendaji aliielezea kamati juu ya historia ya mradi huu uliopendekezwa mwaka 2016/2017, umuhimu wa mradi kwa taifa na utendaji kazi wa mashine. Mkurugenzi mtendaji alieleza kuwa “Mashine hii inahitaji mgonjwa kuwekewa dawa za nyuklia kupitia mshipa wa damu na mgonjwa kuingizwa katika mashine ya PET/CT scan ili kupimwa na kuangalia ugonjwa ulivyoenea mwilini na kuwa pia mradi unahusisha ujenzi wa Jengo la kusimika mashine husika, na vyumba vya kuweka dawa za nyuklia kwa mgonjwa na mradi unahusisha ununuzi wa mashine ya Cyclotron. Hii ni mashine ambayo inazalisha dawa za nyuklia (radioisotopes) ambazo mgonjwa atapatiwa.
Baada ya wasilisho la taarifa ya utekelezaji, kamati ya bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii, ilifanya ziara kutembelea Kutembelea Taasisi na hasahasa kuangalia eneo lililotengwa kwa ajili ya Mradi wa PET/CT scan, kuangalia Huduma za Tiba Mionzi za LINAC na kuangalia Huduma za Nuclear Medicine.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii kwa niba ya wajumbe, aliipongeza sana Serikali ya awamu ya tano na Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa uwekezaji na utekelezaji makini uliozingatia sheria za manunuzi na mikataba. Mwenyekiti alisema kuwa uwekezaji huo wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha kufanya vipimo vya Saratani kwa kutumia PET Scan na ujenzi wa kiwanda cha kuzalishia mionzi dawa ya radio isotopes itaifanya nchi ya Tanzania kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa kimatibabu.
Akielezea kuhusiana na mradi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima alisema, “Serikali inafanya mapinduzi makubwa na makini katika kuhakikisha kuwa ubora wa huduma za afya kwa watu wote zinaimarishwa na kutolewa kwa wakati na ufanisi. Na kwa kuwa magonjwa yasiyoambukiza yana njia za kuzuia ikiwamo kufanya mazoezi, basi amewashajihisha watanzania kujua njia za kujikinga na kufanya mazoezi kwa wingi.