Dc. Jokate ahimiza jamii kutembelea, kuwafariji wagonjwa

      Comments Off on

Dc. Jokate ahimiza jamii kutembelea, kuwafariji wagonjwa

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegero amepokea msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na Jema Foundation kwa ajili ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu ya saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Taasisi hiyo inasimamiwa na Jema Baruani ambaye ni miongoni mwa wagonjwa waliowahi kutibiwa saratani Ocean Road na kupona sasa akijitolea kuendelea kuelimisha jamii kuhusu magonjwa hayo.

Akipokea msaada huo, amehimiza jamii kuendeleza utamaduni wa kuwatembelea, kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa wodini, hospitalini walimolazwa ili kupatiwa matibabu dhidi ya maradhi mbalimbali yanayowakabili.

“Hakuna anayeijua kesho yake,” amesisitiza.

Dc jokate ametumia mfano hai wa shangazi yake ambaye alijiwekea utaratibu wa kuwatembelea na kuwasaidia wagonjwa pasipo kujua kwamba kitendo hicho siku moja kingekuwa msaada mkubwa kwake.

“Alikuwa anajitoa sana, kila alipotoka kazini aliwatembelea wagonjwa wa saratani, sasa hivi ni mstaafu, wakati alipokuwa anafanya vile hakuwahi kufikiri siku moja itakuwa sehemu muhimu ya kipenzi chake (mume wake), kwenda kutibiwa.

“Kwa hiyo, alipolazwa kwa matibabu, kwa kuwa yeye (shangazi) alikuwa tayari anafahamika, ilikuwa wepesi kusaidiwa pia. Tunayoyafanya sasa ni hazina ya maisha yetu ya baadae,” amesisitiza.

Amewapongeza Jema Foundation kwa kujitoa kwa jamii hususan wagonjwa wa saratani kwa kuwatembelea na kuwafariji kila mwaka.

“Nawapongeza madaktari na wataalamu wote wa Ocean Road kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuwahudumia wagonjwa hawa,” amesema.

Ameongeza “Kipekee naipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesimika vifaa vya kisasa hapa Ocean Road na sasa tunashuhudia inapokea wagonjwa wengine pia kutoka nje ya Tanzania.

“Daktari (Crispin Kahesa), amenieleza kwamba wanapokea wagonjwa kutoka nje ya nchi kwa sababu kuna uwezekaji mkubwa umefanywa na Serikali kwa kusimika mashine ambazo wenzetu kwenye nchi zao hawana.

“Amenieleza, huduma za tiba ya saratani zinayopatikana Tanzania ni bora za viwango vya kimataifa na gharama ni nafuu kulinganisha na mataifa mengine.

“Haya ni mambo ambayo lazima tuwaambie Watanzania, wajue kwamba tuna vitu ambavyo wengine wanatamani kuwa navyo, waje wapatiwe huduma bora,” ametoa rai Mkuu huyo wa Wilaya.

Mwakilishi wa Jema Foundation, Jema Baruani amesema wagonjwa wengi wa saratani huwa na hofu pale wanapogundulika, wapo wengine ambao huacha matibabu.

“Si wote huwa na moyo wa ujasiri kama mimi, wapo wanaokata tamaa,  si wote wana uwezo wa kulikabili gonjwa hili, inabidi sisi ambao Mungu ametujalia, tujitoe katika hali na mali, kuwaona… unaweza ukaja hapa japo kuwaambia neno pole, ikawa ahueni kwao,” amesema.

Jema ametoa rai pia kwa jamii hususan vijana kuwa na ujasiri na kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa saratani kwani ikiwa kugundulika, mtu hupona baada ya matibabu.

Mkurugenzi wa Kinga wa ORCI na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, Crispin Kahesa amesema kila mwaka inakadiriwa Tanzania kuna wagonjwa wa saratani zaidi ya 42,060 asilimia 13 ndiyo hufika hospitali ni takriban wagonjwa 12,600.

“Hawa wanaokuja hospitalini asilimia 70 ndiyo huweza kukaa na kuendelea na tiba, asilimia 30 huwa wanakatiza au wanapotea kwa sababu tofauti tofauti ikiwamo mtazamo na hofu waliyonayo juu ya ugonjwa huo.

“Lakini pia kwa sababu huduma hizi zipo mijini zaidi, inawezekana wanapotea kwa kuwa wana majukumu mengi, watu wana changamoto nyingi za kiuchumi na kijamii,” amebainisha.

https://matukionamaisha.blogspot.com/