Waamini wa Kanisa Katoliki Mtakatifu Vincent wa Paulo, Parokia ya Kibamba, wamewashukuru wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), kwa kuwapeleka huduma ya uchunguzi wa afya bila malipo.
Kanisa hilo jana liliadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Vincent wa Paulo ambaye ni somo wa parokia. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya waumini wa kanisa hilo, wamesema kufikishiwa huduma hizo za uchunguzi imekuwa jambo jema kwani wamepima na kujitambua afya zao.
“Tunasherehekea kumbukumbu ya Mtakatifu Vincent wa Paulo, Baba Paroko wetu, aliona vema wataalamu waje kanisani nasi tupate huduma za uchunguzi, nimefarijika mno, nimechunguzwa saratani ya kizazi na matiti bila malipo, nimeambiwa nipo vizuri, nina amani moyoni mwangu,” alisema mmoja wa waumini hao.
Muuguzi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani ORCI, Beatrice Mushi alisema waliwachunguza jumla ya waamini 168.
“Katika idadi hiyo 81 tuliwachunguza saratani ya matiti ambapo wawili tuliwakuta na uvimbe ni kiashiria cha awali cha saratani, 59 tuliwachunguza saratani ya kizazi watatu kati yao tuliwakuta na viashiria vidogo vya saratani na mmoja kiashiria kikubwa,” alisema.
Aliongeza “Kwa upande wa saratani ya tezidume waliochunguzwa ni wanaume 28 ambapo wawili kati yao tuliwakuta na viashiria vya saratani, tuliowakuta na viashiria tumewapa rufaa kuja kule kwenye taasisi yetu kwa uchunguzi zaidi na matibabu.
Awali wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo, Paroko wa Kanisa hilo, Padre Prejo Joseph aliwashukuru wataalamu wote wa afya waliokubali kujumuika nao katika maadhimisho hayo pamoja na wataalamu wa masuala ya kisheria.
https://matukionamaisha.blogspot.com/