Wanaume tisa sawa na asilimia 8 ya wanaume 103 waliojitokeza kwenye kampeni maalum ya uchunguzi wa awali kwa magonjwa ya saratani, wamekutwa na saratani ya tezidume, Mkoani Njombe.
Kampeni hiyo imefanywa na wataalamu mabingwa wa Taasisi ya Saratani Ocean Road {ORCI} ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe kwa siku tatu {April 8 hadi 10} kwa ufadhili wa benki ya NBC., Akizungumza Meneja Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani {ORCI}, Dkt. Maguha Stephano amesema wanaume hao walichunguzwa kwa kipimo cha damu {PSA} na kwamba wamepewa rufaa kufika Ocean Road kwa matibabu zaidi.
Amebainisha kwamba kiujumla watu 600 waume kwa wake walijitokeza kwenye kampeni hiyo kufanya uchunguzi wa afya zao. “Wanawake 497 walijitokeza ni sawa na asilimia 83 ya wote waliofika kwa ajili ya uchunguzi wa afya zao na 103 sawa na asilimia 17 ni wanaume,” amefafanua. Amesema wanawake saba walikuwa na uvimbe kwenye matiti, wawili walikutwa na viashiria vya awali vya saratani ya matiti.
“Wanawake wengine walichunguzwa saratani ya mlango wa kizazi, 10 walikutwa na mabadiliko ya awali (precancerous lesions) na walipatiwa tiba (cryotherapy) ili kuzuia saratani ya mlango wa kizazi. Amesema wanawake wawili walikutwa na saratani ya mlango wa kizazi na kupewa rufaa kwenda Ocean Road.