Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kushirikiana na Tanzania Breast Cancer Foundation, iliandaa Matembezi ya kuadhimisha Mwezi wa kuhamasisha jamii juu ya uelewa kuhusu Saratani ya Matiti.
Oktoba ya kila mwaka, ni mwezi maalumu uliochaguliwa juu ya kueneza elimu na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa uchunguzi wa mapema na njia bora za kuzuia maradhi ya Saratani ya Matiti.
Maadhimisho ya mwaka 2019, yalikuwa na kauli mbiu iliyosema ” Sambaza Ujasiri, Tuna nguvu pamoja, tunashinda (Shared courage, strong together, we overcome) ” na wafanyakazi wa Taasisi ya Saratani waliungana na washiriki wengine mashuhuri katika Matembezi hayo yaliyoanzia The Green, Oysterbay na kumalizikia eneo hilo hilo, huku wakihimiza washiriki na watanzania kiujumla kuwa na mazingatio na tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mapema.
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, inaendelea kuhimiza kwa wananchi wa Tanzania kuwa, uchunguzi wa awali wa Saratani ya Matiti, shingo ya kizazi na tezi dume hufanyika kila siku katika kliniki ya uchunguzi wa awali wa Saratani.
Nyote mnakaribishwa katika uchunguzi wa afya wa mapema na tukumbuke kusambaza ujasiri na pamoja tuna nguvu na tutashinda.