TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD IMEANZA KUTOA HUDUMA YA MIONZI TIBA YA NDANI KWA NJIA YA KISASA (3D INTRACAVITARY BRACHYTHERAPY)

      Comments Off on

TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD IMEANZA KUTOA HUDUMA YA MIONZI TIBA YA NDANI KWA NJIA YA KISASA (3D INTRACAVITARY BRACHYTHERAPY)

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imeanza kutoa huduma ya mionzi tiba ya ndani kwa njia ya kisasa (3D INTRACAVITARY BRACHYTHERAPY) kwa wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.

Hayo yamesemwa wiki hili na Dkt Faraja Kiwanga ambaye ni daktari bingwa wa saratani kutoka kliniki ya Bima (HIC) alipokuwa akiwasilisha maada na kuitambulisha huduma hiyo ambayo imeanza kutolewa katika Taasisi kuanzia mnamo mwezi wa tano mwaka huu 2023.

Huduma hii ni ya kibingwa bobezi ambayo inatumia vifaa vya kisasa kuanzia kwenye kumuandaa mgonjwa, kumuwekea vifaa tiba kwa ajili ya mionzi, kutumia kipimo cha CT scan kuangalia kama vifaa tiba vimekaa mahali pake vizuri, pia kutumia picha za CT scan kufanya kontua kwenye sehemu ambapo ugonjwa upo na kufanya kontua kwenye ogani zinazokaribia eneo linalotakiwa kupata tiba ya kutosha na bila kuathiri ogani zilizokaribu, pia kutumia picha za CT scan kupanga tiba na kufanya mahesabu ya dozi ya mionzi tiba na kuhakikisha kuwa ugonjwa unatibiwa kwa ubora wa hali ya juu.

Akichangia maada hiyo Kaimu Mkuu wa Kliniki ya Bima, Dkt Emmanuel Lugina alisema, huduma hii ni muhimu sana hasa ikizingatia kuwa saratani ya mlango wa kizazi ni Saratani inayoongoza kwa idadi ya wagonjwa, hivyo wahudumu wa afya wanapowaona wagonjwa wajikite katika kuwafanyia uchunguzi (clinical examination) na pia kuweka kumbukumbu (documentation) ili kuweza kupanga aina ya mionzi tiba ambayo itamfaa mgonjwa na pia katika kuongeza tafiti katika eneo hili.

Naye Dkt Nuru Mlagalila alichangia kuwa huduma hii ya mionzi tiba ni muhimu kwa wagonjwa wetu wanaotufikia katika taasisi kwa kuwa wengi wa wagonjwa wanafika katika hatua ya pili na ya tatu, ambapo wakipata huduma hii watapata matokeo mazuri ya tiba.

Huduma hii inatolewa kwa ushirikiano wa daktari bingwa wa saratani (clinical Oncologist), Mfizikia Tiba (Medical Physicist), mtaalamu wa mionzi tiba (Radiation Therapist), na wauguzi (Brachytherapy Nurse).

Huduma hii inapatikana katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Block C kwenye chumba cha Mionzi ya Ndani kila siku kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni Jumatatu hadi Ijumaa.