Jamii yaaswa kutoshiriki kukatiza matibabu kwa wagonjwa wa saratani.

      Comments Off on

Jamii yaaswa kutoshiriki kukatiza matibabu kwa wagonjwa wa saratani.

Jamii imeaswa kuacha kuwakatizia matibabu wagonjwa wa saratani kwa lengo la kuwapeleka kwenye maombi, tiba za asili na waganga wa jadi kwani wanaweza kuwasababishia madhara makubwa zaidi ikiwemo kifo.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt Julius Mwaiselage katika mafunzo kwa mashujaa wa saratani ya matiti yaliyofanyika Taasisini hapo ambapo yanalenga kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya saratani na jinsi ya kujikinga ambapo mwezi oktoba umetengwa mahususi katika kutoa elimu ya saratani kwa jamii.

Dkt. Mwaiselage amewataka waganga wa tiba za asili na watu wa maombezi kutowazuia wagonjwa wa saratani kuendelea kuhudhuria matibabu yao hospitali na pale wanapowapa dawa kushauriana kwanza na Daktari ili ijulikane dawa wanazotoa zinatibu ugonjwa gani.

“Nitoe wito kwa hawa wanaotoa tiba mbadala iwe ni maombi au wanaotangaza kuwa wanadawa za kutibu saratani kuacha kabisa kuwazuia wagonjwa wa saratani kuendelea na matibabu ambayo wanapatiwa na Taasisi ya Ocean Road kwani wanatupa wakati mgumu wa kuwatibu wagonjwa kutokana na kurudi hospitali wakiwa katika hatua ya tatu na nne ambayo ni changamoto kwa mgonjwa kupona”Amesema Dkt Mwaiselage.

Aidha amesema kwa sasa serikali imeboresha huduma za Afya katika Taasisi hiyo ikiwemo upatikanaji wa dawa, na vifaa tiba ikiwemo mashine za kisasa ambapo wagonjwa wanaweza kupata matibabu na kupona kabisa

Ameongeza kuwa kwa sasa huduma ya kutibu saratani ya matiti ambayo inashika nafasi ya pili kwa asilimia 15 kati ya wagonjwa wa saratani elfu 42 kila mwaka inatibika kwa kukuondoa tu uvimbe bila kukata titi lote na kwa waliokatwa titi tayari kuna Madaktari walioenda kupatiwa mafunzo nchini China na wakirudi watawafanyia upasuaji wa kurudisha titi.

Aidha katika mafunzo hayo pia kutatolewa elimu ya jinsi ya kuishi na saratani ndani ya jamii ikiwemo kunyanyapaliwa haswa kwa wale wanaokatwa titi, imani potofu kuwa saratani haiponi na matangazo ya kwenye mitandao ya uwepo wa dawa za kutibu ugonjwa wa saratani kutokana na wagonjwa wa saratani kuchukua mda mrefu kupona kwa kuzingatia taratibu za hospitali.

Hata hivyo amesema huduma za matibabu ya saratani zimeboreshwa katika kipindi hiki cha awamu ya 5 ambapo kila mwaka bajeti ya zaidi ya shilingi Bilioni 7 hutengwa kwa ajili ya dawa za saratani na kusababisha wagonjwa wa saratani kuishi kwa muda mrefu.

Dkt Mwaiselage amesema katika kipindi hiki cha mwezi mmoja cha kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa wa saratani watatoa huduma ya uchunguzi wa saratani na elimu kwa wananchi ili wajichunguze wenyewe pamoja na kuwasisitiza kuwahi hospitali mapema pindi wanapoona dalili za ugonjwa wa saratani.

Sambamba na hayo amesema baada ya kuboresha kwa huduma za Afya katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 wamekuwa wakipokea wagonjwa elfu 55 kila mwaka tofauti na awali walipokuwa wanapokea wagonjwa elfu 33 huku wanaotibiwa na kupona ni asilimia 60 tofauti na awali walikuwa wanapona asilimia 20 tu.

Kwa upande wake Meneja Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani Dkt Maguha Stephen amesema sababu zinazochangia kuongezeka kwa saratani ya matiti ni pamoja na wanawake kutonyonyesha kwa muda mrefu, kuacha kunyonyesha kabla ya miaka 2, aina ya ulaji wa vyakula ikiwemo vile vya mafuta, kupata hedhi mapema na kurithi.

Dkt Maguha amesema ugonjwa wa saratani bado ni tishio Duniani ambapo kila mwaka hupatikana wagonjwa milioni 18 hivyo jamii inapaswa kujilinda dhidi ya ugonjwa wa saratani hususani ya matiti ambayo kwa kiasi kikubwa huadhiri wanawake kwa asilimia 99 na wanaume kwa asilimia 1 kwa kula vyakula vya mboga mboga, samaki kunyonyesha kwa wakati na kufanya uchunguzi wa saratani mara kwa mara.

Nao baadhi ya mashujaa wa saratani waliohudhuria katika mafunzo hayo akiwemo Halima Mwaipopo ambaye ametibiwa miaka 18 sasa kwa kukatwa titi lake amesema kwa sasa anajisikia kupona kabisa na hiyo inatokana na kuzingatia taratibu zote alizokuwa anaelekezwa na Daktari pamoja na kutokata tamaa licha ya unyanyapaa aliokuwa anaupata ndani ya jamii alijipa moyo na kumuomba Mungu.

Shujaa wa Saratani Nyakolema Silla amtoa wito kwa wagonjwa wa saratani kutokata tamaa na kuzingatia hatua zote za matibabu wanazoelekezwa na Daktari pamoja na kukubaliana na hali zao kwani itawasaidia kuishi na jamii bila kujali changamoto za kunyanyapaliwa

Chanzo: https://mtezamedia.wordpress.com/2020/10/01