Mwezi wa Uhamasishaji wa Saratani ya Matiti, unaadhimishwa kote ulimwenguni ifikapo kila Oktoba, maadhimisho hayo hulenga kusaidia kuongeza umakini na msaada wa elimu kwa wanawake, ugunduzi wa mapema na pia huimarisha upatikanaji wa matibabu wa mapema wa ugonjwa huu baada ya kugundulika mapema.
Idara ya kinga na uchunguzi wa Saratani ya Taasisi ya Saratani Ocean Road pia, imeadhimisha mwezi wa uelimishaji wa Saratani ya matiti duniani. Oktoba inafahamika duniani kote kuwa ni mwezi maalumu wa kuadhimisha mapambano dhidi ya Saratani ya matiti.
Idara ya Kinga na Uchunguzi wa Saratani iliaandaa semina maalumu kwa wanawake mashujaa
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Dr. Mwaiselage akizungumza na washiriki wa semina
mnamo tarehe 01/10/2020 lenye dhumuni kuu la kuwapa elimu ya Kinga na ufahamu wa njia stahiki za kujichunguza au kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya Matiti. Ujumbe mkuu wa maadhimisho ya mwezi huu ni ‘Ushirikiano wa pamoja katika kinga na tiba’.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Dr. Mwaiselage akizungumza na washiriki wa semina
Akizungumza na washiriki wa semina, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road alieleza kuwa, Kuna visa vipya milioni 1.38 na vifo 458,000 kutokana na saratani ya matiti kila mwaka (IARC Globocan, 2008) duniani kote. Saratani ya matiti ni saratani ya kawaida kwa wanawake ulimwenguni kote, katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea. Katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati matukio yamekuwa yakiongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuongezeka kwa umri wa kuishi, kuongeza ukuaji wa miji na ubadilikaji wa mitindo ya maisha kama ilivyo nchi za magharibi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Dr. Mwaiselage akizungumza na washiriki wa semina
Hivi sasa kuna ujuzi wa kutosha katika ugunduzi na tiba za saratani ya matiti, hata hivyo, kugundua mapema ugonjwa huo ni sababu kuu na ya msingi katika kudhibiti na kuitibu saratani ya matiti. Ikiwa saratani ya matiti inagunduliwa mapema, na ikiwa utambuzi na matibabu ya kutosha yanapatikana, kuna nafasi nzuri kwamba saratani ya matiti inaweza kuponywa na mgonjwa kuendeleza kuishi katika hali ya kawaida kabisa.
Dr Mwaiselage alitumia semina hilo, kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli kwa kutekeleza kivitendo mipango kamili ya kudhibiti saratani kwa ununuzi wa vifaa tiba na sapoti inayoendelea katika miradi mipya na hali ya upatikanaji wa dawa za kutibu Saratani nchini na hasa hasa katika Hospitali ya Ocean Road
Wakizungumza na washiriki, watoa mada katika semina, Sister Mary Haule na Sister Genoveva Mlewa waliwaasa wanawake wote kujenga utaratibu wa kupima mapema. “Ikiwa itachelewa kugunduliwa, hasa inapokuwa katika hatua ya tatu na nne, hapo hulazimika kutibiwa kwa matibabu ya tiba shufaa, ambapo, utunzaji mzuri wa kupunguza mateso ya wagonjwa na familia zao hufanyika”. Kwa msingi huo, waliwaasa wanawake wote, kuweka utaratibu wa kujichunguza na kufika hospitalini mapema kuweza kuchunguzwa, na ili wanapobainika wapatiwe matibabu ya haraka na yenye manufaa
Akiongelea kuhusu madhara ya vifo, Mkurugenzi wa Idara ya Kinga na Uchunguzi, Dr Crispin Kahesa alisema, ”Vifo vingi (269,000) vinatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ambapo wanawake wengi walio na saratani ya matiti hugunduliwa katika hatua za mwisho kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu juu ya kugundua mapema na vizuizi vya huduma za afya kwa mapema. Aliendelea kuwahimiza kina mama, kuratibu na kuhudhuria kliniki za uchunguzi wa Saratani mara kwa mara ili kujiepusha kuja kugundulika katika hatua za mwisho.
Mkurugenzi Idara ya Kinga, Dr. Kahesa akizungumza na washiriki wa semina
Katika maadhimisho ya mwezi huu, Taasisi ya Saratani Ocean Road, itaendelea na programu za uchunguzi na tiba za Saratani ya matiti kwa wanawake wote watakaofika katika kliniki ya uchunguzi na tiba iliyopo jengo la Block A. Tunawahimiza kwa wanawake wote kujumuika na kushirikiana na wahudumu wetu ili wapate kuchunguzwa na kujua mustakbali wa afya zao.
Upasuaji kuondoa uvimbe wa saratani bila kuondoa titi lote waleta ahueni kwa wagonjwa
Upasuaji wa kisasa wa kuondoa uvimbe wa saratani pasipo kuondoa titi lote lililoathirika umeleta ahueni kwa wagonjwa na kupunguza unyanyapaa nchini.
Yameelezwa hayo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Julius Mwaiselage alipozungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalum, kuhusu mwezi Oktoba ambao ni maalum Kidunia kwa ajili ya uelimishaji, uhamasishaji, uchunguzi na matibabu ya saratani hiyo.
Mashujaa (wanawake waliotibiwa na kupona saratani ya matiti) na wale wanaoendelea na matibabu dhidi ya ugonjwa huo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI Dk Julius Mwaiselage pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za kinga ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dk Crispin Kahesa wakiinua Mkono juu kuashiria kuishinda Saratani ya matiti
Amesema wastani wa wanawake 100 wanaogundulika na saratani hiyo ikiwa katika hatua za awali, huondolewa uvimbe kwa njia ya upasuaji pasipo kung’olewa titi lote lililoathiriwa, kila mwaka.
Amesema huduma hiyo ilianza kutolewa rasmi mwaka 2016 nchini na wataalamu wa ORCI wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH- Mloganzila).
Dk. Mwaiselage amebainisha kwamba ORCI kila mwaka huona wagonjwa wa saratani ya matiti kati ya 600 hadi 700 ambapo hao 100 ambao ni sawa na asilimia 30 hutibiwa kwa kuondoa uvimbe pasipo kung’oa titi lote.
“Zamani kwa kuwa hatukuwa na mashine za kisasa za tiba mionzi, matibabu yalikuwa ni lazima kuondoa titi lote, changamoto nyingine tuliyokuwa tunakabiliana nayo ni wagonjwa hawa kuchelewa kuja hospitalini, walikuja ugonjwa ukiwa umefikia hatua za juu mno, haikuwa rahisi kupata matokeo mazuri ya tiba.
Mashujaa (wanawake waliotibiwa na kupona saratani ya matiti) na wale wanaoendelea na matibabu dhidi ya ugonjwa huo wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI Dk Julius Mwaiselage (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao
“Lakini kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa kutumia mashine hii ya ‘Linear accelerator’, tunao uwezo wa kuchunguza na kutibu kwa kuondoa ule uvimbe tu na kuliacha titi, baada ya upasuaji huo mgonjwa anaendelea na matibabu ya mionzi kupitia mashine ya kisasa tuliyonayo hapa ORCI,” amesisitiza.
Amesema hata wale waliofanyiwa upasuaji na kuondolewa katika titi lote jitihada zinafanyika ambapo tayari wataalamu wapo nchini China wakijifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kupandikiza matiti.
“Corona imetuchelewesha, walikuwa wawe wameshamaliza masomo yao na kurejea nchini tayari kuanzisha huduma hii,” amebainisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratni Ocean Road, Dk Julius Mwaiselage akizungumza na mashujaa hao
Amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kila mwaka Tanzania kuna wagonjwa wapya 42,000 wa saratani aina zote, saratani ya matiti inaongoza duniani kote kwa kuathiri wanawake kwa asilimia 99, wanaume asilimia moja.
“Tanzania saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa idadi kubwa ya wagonjwa, miaka 10 iliyopita ilikuwa inashika nafasi ya nne, tunaona inaongezeka kwa kasi,” amebainisha.
Amesema changamoto ambayo wanaiona hivi sasa kwenye jamii ni wimbi la taarifa potofu zilizopo kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wagonjwa hushawishiwa kwenda kupata dawa za kienyeji ambazo hata hazijafanyiwa utafiti na hivyo huacha tiba za hospitalini.
Mkurugenzi wa Huduma za kinga ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dk Crispin Kahesa akizungumza jambo katika semina ya siku moja kwa mashujaa wa saratani ya matiti.