Tiba ya mionzi inayotolewa na wataalamu wa magonjwa ya saratani si tanuru la moto kama ambavyo baadhi ya watu kwenye jamii wamekuwa wakidhani na kusambaza taarifa hizo zisizo sahihi.
Daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Kandali Samwel amesema hayo wakati wa alipokuwa akizungumza na walimu, wafanyakazi na wanachuo wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA (ICT- Kipawa.
“Tunaona baadhi ya wagonjwa tunaowahudumia kule Ocean Road, tukiwaeleza wanatakiwa kupata tiba mionzi wanakataa, unasikia mgonjwa anasema ni kule wanakoingizwa kwenye tanuru la moto, jamani si kweli kwamba tiba ya mionzi ni tanuru la moto,” amesema.
Amesema tiba mionzi dhidi ya saratani imehakikishwa ni salama na kwamba haina uwezo wa kuunguza mwili kama vile tanuru liwakavyo na kuunguza.
“Jamii ielewe, ni tiba sahihi iliyohakikishwa usalama wake na tiba hii si kwamba daktari mmoja anaamua kumtibu mgonjwa, kumchukua na kwenda kumuingiza katika chumba cha matibabu, hapana!.
“Daktari anapopendekeza, kuna jopo la wataalamu sita wanaosimamia matibabu hayo, ni wataalamu wa fani mbalimbali wanaojumuika katika kutoa tiba hiyo kwa kila mgonjwa mmoja.
“Kuna hesabu mahususi ambazo hupigwa, wanafanya ‘calculation’ kulingana na mgonjwa husika, si kila mgonjwa atapewa mionzi aina hiyo hiyo, wanaangalia ugonjwa upo sehemu gani, umefikia hatua gani na mambo mengine mengi,” amesisitiza.
Amesema jambo la muhimu kwa jamii kuzingatia ni kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kuweza kubaini iwapo wanakabiliwa na magonjwa ya saratani au la ili kugundua mapema na kupata matibabu mapema.
“Tunaona zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanaokuja kule Ocean Road wamechelewa matibabu, inafanya ugumu hata katika kuwapa matibabu, ugonjwa unakuta upo hatua za juu, tunahimiza kufanya uchunguzi wa awali mapema,” ametoa rai.
Amesema katika kuadhimisha mwezi wa Oktoba, ambao ni mahususi kwa uelimishaji kuhusu ugonjwa wa saratani ya matiti, waliona vema kwenda kuzungumza na walimu, wafanyakazi na wanachuo wa VETA ICT- Kipawa. “Tumewapa elimu sahihi, maana kuna taarifa nyingi zisizo sahihi kwenye jamii, sambamba na elimu pia tunafanya uchunguzi wa awali, wale tutakaowakuta na tatizo tuweze kuwapa matibabu mapema na wengine wajue jinsi ya kuendelea kujikinga wasipate maradhi haya,” amebainisha