Maelfu wafika ofisi za Efm & TV E kuchunguzwa saratani ya matiti

      Comments Off on

Maelfu wafika ofisi za Efm & TV E kuchunguzwa saratani ya matiti

Mwamko wa wananchi kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti unazidi kuongezeka kwenye jamii hadi kwa kundi la wanaume.

Leo katika Ofisi za Efm na TV E zaidi ya watu 1,000 wamejitokeza kuchunguza afya zao ambapo kati ya hao wanaume ni zaidi ya 100.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa, amesema hiyo inaonesha wazi kwamba elimu juu ya magonjwa ya saratani inazidi kufika kwenye jamii.

Amesema saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaowaona na kuwatibu Ocean Road na kwamba kwa mwaka takriban wagonjwa 800 huwa ni wenye saratani ya matiti.

“Mwezi Oktoba, kila mwaka duniani ni mahususi kwa ajili ya uelimishaji na uchunguzi wa saratani ya matiti, ili kuweza kuwagundua na kuwatibu mapema wagonjwa.

“Ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha, ORCI tumeshirikiana na Efm na TV E katika kuhitimisha kampeni ambayo tumeifanya mwezi mzima. Kampeni hii imetutia moyo, tunashukuru vyombo vya habari vimetusaidia…

“Si kitu cha kawaida kina baba kujitokeza kwa wingi namna hii hasa maeneo ya mijini ikizingatiwa pia ni mwisho wa wiki, hapa tumeweka vituo sita vya kufanya uchunguzi wa awali, vifaa na wataalamu tupo,” amesema.

Ameongeza “Tunapenda kuhamasisha jamii washiriki uchunguzi wa awali ni bure kwa wale ambao hawatapata fursa kushiriki hapa leo,  tunawakaribisha kufika ORCI kule tunaendelea kutoa huduma hii kila siku.

Dk. Kahesa ambaye pia ni Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani amesema huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti zinapatikana nchi nzima ambapo Serikali imeweka mtandao wa vituo zaidi ya 700.

“Ocean Road ina wabobezi na vifaa vingi na huwa tunafanya huduma hizi za mkoba tunaifikia jamii kwenye makazi yao, tunatoa elimu kuhusu visababishi vinavyoweza kuongeza hatari ya mtu kupata saratani, tunahamasisha Jamii kujenga tabia ya kuchunguza mara kwa mara.

“Kwa sababu inaweza kugundua mapema na inapogundulika mapema inatibika na mtu kupona kabisa, sasa hivi Tanzania tunao mashujaa waliotibiwa na kupona baada ya miaka 20,” amebainisha.

Naye, Daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Kandali Samwel, amesema ingawa tafiti zinaonesha wanawake ndiyo huathiriwa zaidi na saratani ya matiti, inapowaathiri wanaume huwa kali kidogo.

“Kitaalamu tunasema inakuwa addresive’ yaani inasambaa kwa haraka zaidi kuliko kwa wanawake, kwa sababu

mwenendo wa matibabu yao huwa tofauti na wanawake,” amesema.

Ameongeza “Hamasa kubwa tunayosisitiza ni watu kuchunguza mapema ili kuokoa maisha, kwani ikigundulika mapema inatibika na kupona kuliko mtu anapochelewa.

“Changamoto kubwa tunayoiona kwenye Taasisi yetu ni watu kufika wakiwa wamechelewa na ugonjwa ukiwa upo katika hatua za juu,” amesema Dk. Kandali.

Meneja Mkuu wa Efm na TV E, Mohamed Lukwili amesema huo ni mwanzo wa ushirikiano kati yao na Ocean Road katika kuifikia jamii.

“Tulianza ushirikiano baada ya sisi wafanyakazi wa Efm na TV E kwenda Ocean Road, kufanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani, tukaona isiishie pale kwa sababu vyombo vya habari vinatazamwa kama muhimili wa nne kwenye nchi yetu, tunasikilizwa na wengi, maana yake tuna nafasi kubwa kushawishi watu wafahamu hali zao.

“Hivyo, leo  tumewakusanya wanaume kwa wanawake ili wapate nafasi ya kupima saratani ya matiti na tezidume kwa wanaume, tangu saa mbili asubuhi hadi kufikia saa tisa jioni, tumeandikisha watu wapatao 1,400, lengo letu ni kuwezesha wengi zaidi wafanya uchunguzi hata wakifika 2,000 tutawahudumia.

“Kwa sababu tunafahamu saratani ni ugonjwa unaotesa ndugu zetu wengi Tanzania, tunapopata wananchi wengi zaidi inamaanisha waligundulika mapema tutakuwa tumeokoa wengi zaidi,” amesema.

Ameongeza “Mwamko ni mkubwa wamefika hata wenye umri wa miaka chini ya 18 jamii imeelimika kwamba magonjwa haya si tu yanatesa wazee bali hata watu wa rika nyinginezo wanaathirika.