Wanachuo zaidi ya 200 Veta (ICT – Kipawa) wafikishiwa elimu saratani ya matiti

      Comments Off on

Wanachuo zaidi ya 200 Veta (ICT – Kipawa) wafikishiwa elimu saratani ya matiti

Wanafunzi wakisikiliza kwa makini wakati Dk. Kandali akiwasilisha mada

Wanachuo zaidi ya 200 wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta (ICT- Kipawa wamepewa elimu sahihi kuhusu saratani ya matiti, jinsi ya kujikinga, uchunguzi na matibabu.

Elimu hiyo imetolewa leo na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), waliofika chuoni hapo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha mwezi wa Oktoba ambao kidunia ni maalum kwa ajili ya uelimishaji kuhusu saratani hiyo.

Akizungumza na wanachuo hao, Daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Kandali Samwel amewahimiza kuepuka visababishi vinavyoweza kuwapelekea kupata saratani hiyo ikiwamo mtindo usiofaa wa maisha kama vile unywaji wa pombe na uvutaji sigara, kutokufanya mazoezi na matumizi ya vyakula vyenye chumvi na sukari kwa wingi.


“Saratani hii kwa asilimia 99 inawapata wanawake na kwa asilimia moja wanaume, ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kila mwaka kwa kuwaona wataalamu kujua iwapo umepata saratani hii au la, ili pia kugundulika mapema na kupatiwa matibabu mapema,” ametoa rai.

Ameongeza “Kwa sababu ikigundulika mapema inatibika, lakini mtu akichelewa matibabu yake huwa hayatoi matokeo chanya, zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanaokuja pale ocean road wamechelewa kugundulika.

Daktari huyo amewasihi wasichana kujiepusha na matumizi holela ya muda mrefu, pasipo kuzingatia ushauri wa daktari, kwa wingi kupita kiasi kwa vidonge vya dharura vya kuzuia mimba maarufu P2, kwani ni tabia hatarishi inayoonekana kuchangia kupata saratani hiyo.

“Pale Ocean Road miaka ya hivi karibuni tunagundua hadi wasichana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 25 wana saratani ya matiti,  wapo wanaoeleza wametumia dawa hizo bila ushauri wa daktari, kwa wingi na kwa muda mrefu.

“Hata hapa chuo baadhi yenu wametueleza hivyo. Tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani zinaonesha watu wanaotumia holela, kwa wingi vichocheo hivyo wapo kwenye uwezekano mkubwa kuishia kupata saratani hiyo.

“Hivyo, tunapata hizo taarifa, tunatilia maanani na tunaendelea kutoa elimu sahihi ili mbeleni tusije tukapata shida, hii inatufumbua macho na huu ni wito kwa kwa upande wa tafiti tuangalie shida hii ipo kwa kiwango gani kwenye jamii.

“Sisi tunaona tu kama wahudumu watu wanatoa hizi shuhuda, lakini hatuwezi kujua kwa kiwango gani pengine tatizo ni kubwa zaidi, hili linaweza kuletewa majibu na tafiti za kisayansi zaidi.

“Kimsingi dawa hizi zinapaswa kutumiwa pale tu dharura inapotokea ndiyo maana zinaitwa ‘emergency contraceptive’,  zimewekwa kwa ajili ya dharura na dharura kutokea labda ni mara moja, kwa mfano kwa mtu ambaye anaweza kujamiiana pasipo kutarajia kile kitendo labda amebakwa na sisi wataalamu tunatarajia kitendo hicho si cha mara kwa mara.

Amesema njia za uzazi wa mpango zina kiwango cha homoni ambazo zinakuwa zimepimwa kwa wakati huo, lakini kumbe jamii wanafanya kuwa matumizi ya mara kwa mara, kwa wingi bila ushauri wa wataalamu, wanameza kama karanga.

Amesema pamoja na hilo, vipo visababishi vingine vinavyoweza kuchangia mwanamke kupata saratani ya matiti ikiwamo kuchelewa kuzaa, kutokuzingatia kunyonyesha ipasavyo, kurithi kwenye familia na sababu nyinginezo.

Awali, Kaimu Meneja Rasilimali Watu Veta- ICT Kipawa, Upendo Abraham ameshukuru wataalamu wa ORCI kufika chuoni hapo na kuelimisha wanafunzi na watumishi wake kuhusu saratani hiyo.




“Kwa sababu asilimia moja ya wanaopata saratani hii ni wanaume na asilimia 99 ni wanawake, tuna vijana hapa tuliona wakielimishwa kuhusu visababishi vya saratani hii elimu hii, itawasaidia na wale watakaokutwa na tatizo watapata matibabu kwa wakati.

“Wanafunzi 124 na watumishi 24 wakiwamo wanaume wameonesha utayari wa kuchunguzwa, hapa chuo wanafunzi wetu wengi ni wanaume kwa asilimia 75,” amesema.

Naye Miss Utalii wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sarafina Sisse amesema elimu hiyo imetolewa kwa wakati sahihi kwa kundi sahihi hilo la vijana kwani itawasaidia kujitambua na kuwahi kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.

Miss utalii wa Mkoa wa Dar es salaam, Sarafina Sise akizungumuza na wanafunzi hao

“Ni jambo zuri walilofanya na mimi jukumu langu kubwa ni kuhamasisha jamii kupitia elimu hii, wanafunzi watatoka na kwenda kuwafikishia wengine kwa upana zaidi,” amesisitiza.

Wanafunzi Christina Steven na Steven Danford wameomba wataalamu hao kuendelea kutoa elimu kwa jamii hususan mashuleni ili wapate elimu sahihi itakayowasaidia kuepukana na ugonjwa huo.






Pamoja na wanachuo hao, wataalamu wa Ocean Road awali walizungumza pia na walimu na watumishi wa Chuo hicho na kuwapatia elimu juu ya ugonjwa huo.