UJUMBE KUTOKA BURUNDI WATEMBELEA TAASISI YA SARATANI KWA AJILI YA MAFUNZO

      Comments Off on UJUMBE KUTOKA BURUNDI WATEMBELEA TAASISI YA SARATANI KWA AJILI YA MAFUNZO

Ujumbe wa wataalamu watano wakiwemo Madaktari na maafisa kutoka Wizara ya Afya ya Burundi upo nchini kwa ziara maalumu ya siku tano kujifunza mambo mbalimbali ya utendaji na uendeshaji unaofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ikiwemo namna inavyotoa huduma zake za matibabu kwa wagonjwa wa Saratani kwa ubora Ukanda wa Afrika Mashariki.

Ujumbe huu maalumu, unalenga kuitumia safari hii ya mazfunzo kwa ajili ya kuja kuanzisha hospitali kama ya Ocean Road pindipo wakirejea nchini Burundi.

Awali akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Julius Mwaiselage amesema wameupokea ujumbe huo kutoka Burundi na utakuwa nchini kwa siku tano kujifunza ili kupata uzoefu ambapo nao wakiwa mbioni kuanzisha huduma kama hizo nchini mwao. Wataalamu hao, walikaribishwa na mwenyeji wao, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dr Julius Mwaiselage, ambaye aliwakaribisha na kuwaeleza kuwa Taasisi kama wawakilishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wana fahari kubwa kuwa wakufunzi wa timu hiyo kutoka Burundi, na kuwa wataalamu wa Taasisi watatumia muda huo wa siku tano kuweza kuwafunza masuala mtambuka yatakayowawezesha na wao wakirudi kwao waweze kuanzisha huduma za matibabu ya saratani.

Mkurugenzi aliwaarifu kuwa, tayari kuna programu za mafunzo ya madaktari na wataalamu wa onkolojia inayoendeshwa kwa kushirikiana na chuo kikuu cha tiba cha MUHAS. Hivyo watumie fursa hiyo kuwaleta wanafunzi kuja kujiunga na programu hizo

Ugeni huo pia utapata nafasi ya kujifunza kwa nadharia na vitendo ambapo watazunguka katika kujionea jinsi huduma zinavyotolewa na namna wanavyoendesha matibabu ikiwemo kutumia mitambo ya kisasa inayotumia miale ya mionzi, mashine ya Linac Accelerator inayopatikana Tanzania pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

 “Kama inavyofahamika ukanda huu wa Afrika hususani Tanzania, ORCI imepiga hatua kubwa sana katika utoaji wa huduma za saratani kwa wananchi wake.

“Hivyo Shirika la IAEA limeona ni busara sana kwa zile nchi ambazo zinataka kuanzisha huduma zake za saratani, zifike Tanzania hapa kwetu ili kujifunza mambo mbalimbali ambayo yamefanyika kwa weredi na kwa upana mkubwa mno,” amesema.

Ameongeza “Ujumbe huu utajifunza pia  tulivyofanya kwa kupitia uboreshaji wa huduma kutibu saratani kwenye vituo, uboreshaji wa tiba  ya kutibu kwenye Kanda, na uboreshaji wa Ocean road kupitia kununua mashine mpya.

“Pia uboreshaji wa tiba kemia, upatikanaji wa dawa pamoja na mafunzo kwa watumishi wa Afya katika utoaji wa huduma ya saratani,” amesema Dk. Mwaiselage.

Amesema sasa wanatarajia kuendelea kupokea ugeni mwingine kama huo kutoka nchi mbalimbali zikiwemo za Liberia na Lesotho amabazo zitafika nchini kujifunza juu ya utoaji na tin ya Saratani.

Dk. Mwaiselage ameipongeza Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kuwezesha taasisi hiyo kiasi kwa sasa imekuwa kimbilio kwa nchi nyingi ambazo zinataka kuja kujifunza namna ya tiba ya Saratani.

“Kwa kipindi hiki cha miaka minne taasisi imekuwa mbele sana katika utoaji wa huduma na nchi nyingi imeona Tanzania tukipiga hatua kwenye kutibu saratani ikiwemo kununua mashine hizi mionzi za kisasa za LINAC ambazo zinapatikana katika nchi chache sana za Afrika huku zikipatikana nchi chache za Ulaya, India na Marekani,” amesema.

Amesema wamejitahidi katika upatikanaji wa dawa za saratani ambazo zinapatikana kwa kiwango kikubwa sana na wagonjwa wanatibiwa vizuri.