Mkurugenzi Ocean Road akemea unyanyapaa kwa wanawake walioondolewa matiti kutibu saratani

      Comments Off on

Mkurugenzi Ocean Road akemea unyanyapaa kwa wanawake walioondolewa matiti kutibu saratani

Na Mwandishi Maalum (ORCI) – Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road {ORCI}, Dk. Julius Mwaiselage amekemea tabia ya baadhi ya wanajamii kuwanyanyapaa wagonjwa wa saratani hasa waliofanyiwa upasuaji wa kuondoa matiti ikiwa ni sehemu ya kufanikisha matibabu dhidi ya saratani hiyo.
Amekemea tabia hiyo mapema leo alipokutana na wanawake wapatao 30, mashujaa wa saratani ya matiti {waliogundulika, kutibiwa na kupona na wale wanaoendelea na matibabu dhidi ya saratani hiyo}.
Amekutana nao kwenye viunga vya Taasisi hiyo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Mwezi wa Saratani ya Matiti {Oktoba} unaobeba dhima ya kuelimisha jamii na kuhimiza uchunguzi wa mapema ili kupata matibabu mapema, ulimwenguni.


“Jamii ielewe kuondolewa titi mwanamke haimaanishi u-‘u-namke’ wake umebadilika, bado upo vile vile na maeneo mengi kama mwanamke anayefanya ataendelea kuyafanya bali ni kiungo hiki kimoja tu ambacho tumekiondoa,” amesema.
Amesisitiza kwamba saratani ya matiti inaathiri pia wanaume ijapokuwa kwao ni kwa kiwango kidogo cha asilimia moja tu na wanawake walichukua asilimia 99.
Amesema ndani ya taasisi hiyo saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa baada ya saratani ya kizazi inayoshika nambari moja.
“ORCI tumeanza kutoa matibabu ya saratani mbalimbali nchini tangu mwaka 1996, kufikia sasa saratani ya kizazi inaongoza kwa asilimia 35, kisha matiti kwa asilimia 15, ukijumlisha idadi yote hii ni karibu asilimia 50, saratani zinazoshambulia wanawake zinaongoza kwa idadi ya wagonjwa,” amedokeza.
Dk. Mwaiselage amesisitiza mapambano dhidi ya saratani ya matiti yanahitaji msukumo zaidi kukizuia isizidi kushambulia jamii kwani takwimu za taasisi hiyo zinaonesha miaka 10 iliyopita ilikuwa inashika nafasi ya nne kwa idadi kubwa ya wagonjwa lakini sasa inashika nafasi ya pili.
“Ni tatizo linaloongezeka, nawashukuru wadau mbalimbali wanaotusaidia kuhamasisha na kuelimisha jamii hasa mashujaa hawa wanahimiza wengine wajitokeze kufanya uchunguzi mapema ili wapate matibabu mapema wanapogundulika,” amesema.
Ameongeza “Serikali imeongeza miundombinu kwenye tiba na Kinga pia elimu inatolewa ili wananchi waelewe dalili na watibiwe hatua za awali, huduma za uchunguzi pia zimeenea nchini.
Amesema nchi nzima vituo zaidi ya 800 vinavyofanya uchunguzi wa saratani ya kizazi na matiti na kwamba upatikanaji wa dawa za kutibu saratani ni mkubwa na umeimarika ka kiwango cha asilimia 98
“Hospitali zetu za Kanda ikiwamo Bugando, KCMC, Mbeya {MZRH}, Benjamin Mkapa na nyingine za binafsi huduma za uchunguzi wa saratani zinafanyika na zimekuwa bora katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kufikia sasa,” amesisitiza.
Ameongeza “… ni kuchunguza na kutibu mgonjwa, kubwa kumshukuru MUNGU sisi tunatibu yeye anaponesha kabisa

anatusaidia.
Amesema pamoja na unyanyapaa changamoto nyingine inayowakabili wagonjwa hao ni imani potofu ambazo huwarudisha nyuma na baadhi yao kuacha kuzingatia matibabu.
“Wengi hufika ugonjwa ukiwa katika hatua za juu mno, Tanzania tuna huduma ya kuondoa vivimbe vya saratani pasipo kuondoa titi lote lakini Kwa sababu wengi huchelewa ndiyo maana wanalazimika kuondolewa titi lote, ndiyo maana tunahimiza mtu awahi kufanya uchunguzi mapema kwani ikiwahiwa hatua za awali ni rahisi kutibila pasipo kuondoa titi lote,” amesema.
“Hivyo, siku kama leo, tunakutana na kujadili ni njia bora zaidi katika kutatua, duniani saratani ya matiti inaongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa, ni muhimu kutoa elimu kwa jitihada mbalimbali na kwa kushirkiana katika kuzuia na kutibu vizuri zaidi,” amesisitiza.
Mashujaa hao hii leo pia wamepatiwa zawadi mbalimbali ikiwamo kanga, pochi na taulo za kike na Klabu ya Lions pamoja na benki ya.. ikiwa ni sehemu ya kusherehekea na kuwapa faraja kwamba hawapo peke yao katika mapambano hayo.