Teknolojia: Vitanda vya kisasa vya umeme, matibabu kwa wagonjwa Ocean Road

      Comments Off on

Teknolojia: Vitanda vya kisasa vya umeme, matibabu kwa wagonjwa Ocean Road

Vitanda viwili vilivyoundwa kwa teknolojia ya kisasa, vikitumia nishati ya umeme, inayosaidia kurahisisha na kuchochea ufanisi wa matibabu kwa wagonjwa waliolazwa wodini, vimekabidhiwa kwa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).
Msaada huo umetolewa na Kampuni ya Gama Pharmaceutical {T} Limited kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Czech kupitia Ubalozi wake nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya msaada huo mapema hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage amesema umegharimu kiasi cha Dola 8000 ambazo ni wastani wa kati ya Sh. milioni 17.
“Utaona ni gharama kubwa, ni vya kisasa sana, ukienda hospitali zozote za kisasa duniani utaona vitanda vya namna hii,” amesisitiza.
Amesema kukabidhiwa kwa mashine hizo kunaifanya taasisi hiyo kuwa na jumla ya vitanda vinane vinavyotumia teknokojia ya kisasa.
“Ni maalum kwa ajili ya kuhudumia wale wagonjwa wanaokuwa wanaumwa sana wodini, tuna vitanda 25, vingine vinatumia njia mbalimbali kwa nguvu ya kupandisha na kushusha.
“Kupata vitanda hivi viwili vya kisasa leo inafanya tunakuwa na jumla ya vitanda vinane vya kisasa kati ya hivyo 25, kwa hiyo vinakuwa rahisi kwa mhudumu na mgonjwa mwenyewe.
“…  anaweza kushusha na kupandisha kulingana na hali atakayokuwa naye, kwa maana hiyo tuna uhitaji wa vitanda 17 vya kisasa vinavyotumia umeme,” amesema.
Ameongeza “Nimeomba kampuni hii ya kitanzania ambayo  imeshirikiana na serikali ya Czech itusaidie tupate vitanda vingine.
Dk. Mwaiselage amebainisha kwamba idadi ya wagonjwa wa saratani nchini inazidi kuongezeka hivyo ni muhimu pia kuzidi kuimarisha huduma za matibabu.
“Karibu asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa wa saratani nchini wanakuja hospitalini katika hatua za juu za ugonjwa, kama wakitibiwa wanakuwa katika hali ‘seriously’ au karibu wanahitaji huduma za namna hii,” amesema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Gama Pharmaceutical, Qutibal Salaheldeen Ahmed amesema kampuni hiyo imeridhishwa na mazingira rafiki ya uwekezaji nchini Tanzania na kwamba kampuni hiyo inajivunia kutoa msaada huo na ipo tayari kuendeleza ushirikiano.Balozi wa Czech – Tanzania, Martin Klepetko amesema nchi hiyo ipo tayari kuendeleza ushirikiano wake na Tanzania katika kuimarisha na kuboresha maeneo mbalimbali kwenye sekta ya afya.
Balozi Dk. Abdalah Posi ameshukuru kwa msaada huo akisisitiza kwamba jambo hilo {ushirikiano huo} ni jema.

“Teknolojia inakua kwa kasi anapokuja mtu kuamua kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa mchango kwa vitu hivi , ni jambo jema, inasaidia kuboresha sekta ya afya na kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Posi.Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza cha Wizara hiyo, Dk. Omary Ubuguyu amebainisha kwamba uhitaji wa vitanda vya namna hiyo nchini bado ni mkubwa.
“Hospitali zetu zote za rufaa za kanda na Taifa vina uhitaji wa vitanda vya namna hii katika maeneo tunayotoa huduma za dharura, ICU na kama hizi za saratani na mengineyo,” amesema.
Dk. Ubuguyu amebainisha mahitaji ya jumla ya vitanda hivyo si chini ya 100 kwa nchi nzima.
“Mahitaji yapo mengi, tunaenda hatua kwa hatua ocean road sasa imefikisha vitanda vinane, hili la msaada wa Gama na Czech sisi inatuamsha zaidi kwamba sasa tunaweza kununua moja kwa moja kutoka kwa mzalishaji na hili ndilo jambo la msingi tulilolifurahia,” amesema.