Mkurugenzi wa huduma za Tiba kutoka wizara ya Afya Prof. Paschal Rugajo, (Picha ya kwanza kushoto) mapema leo ametembelea katika kituo kipya kilichosimikwa mashine za Cyclotron pamoja na PET-CT SCAN na kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo na usimikaji namna unavyoendelea
Akizungumza katika matembezi hayo Prof. Rugajo amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo huku akiuomba uongozi kusimamia kwa umakini ili kituo hicho kiweze kukamilika mapema na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza zaidi, Prof. Rugajo amewataka viongozi kuhakikisha wanatuza rasilimali hizo ili zije kuwafaa watanzania na kuepukana na ugonjwa wa Saratani ambao katika kipindi cha hivi karibuni umeshika kasi katika kupoteza maisha ya Watanzania wengi sana
Kwa upande wake mkurugenzi wa kinga wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Crispin Kahesa, amemshukuru Prof. Rugajo kwa kuweza kupata muda na kutembelea katika jengo hilo na kumuahidi kuwa matumizi ya mashine hizo hayatochukua muda mrefu kuanza ili kuweza kuleta mabadiliko chanya katika Tasnia ya uchunguzi na matibabu ya Saratani nchini
Aidha Dkt. Kahesa amemuhakikishia Prof. Rugajo kuwa mashine hizo zitabaki kuwa salama na zitatoa huduma kwa mujibu wa zinavyotakiwa kutoa kwani Taasisi imejipanga kuhakikisha kuwa inaendana na Sera ya nchi katika kutokomeza magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa huu wa Saratani mbalimbali
Wakati huohuo Dkt kahesa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuchagua kuwekeza kwenye afya kwa kiasi kikubwa, hasa kwa kuziwezesha Taasisi za kiserikali kuweza kutoa huduma za Afya hapa nyumbani kwa urahisi zaidi ili kupunguza rufaa zinazogharimu pesa nyingi za watanzania ambao wengi wao huishia kupoteza maisha kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu nje ya nchi.
Mashine ya PET-CT Scan ni mashine yenye uwezo wa kugundua Saratani katika hatua za awali kabisa na hivyo kurahisisha matibabu na kuepuka madhara makubwa kwa watanzania hivyo kuwaepusha kufika hospitali wakiwa katika hatua za Tatu au nne ambazo ndio hatari sana kwani matibabu yake Yana changamoto za gharama ukilinganisha na yale ya hatua za mwanzo kabisa