SERIKALI IMETOA RAI KWA JAMII KUCHUKUA HATUA ZA MAPEMA KUPIMA UGONJWA WA SARATANI

      Comments Off on

SERIKALI IMETOA RAI KWA JAMII KUCHUKUA HATUA ZA MAPEMA KUPIMA UGONJWA WA SARATANI

SERIKALI imetoa rai kwa jamii kuchukua hatua za mapema kupima ugonjwa wa saratani, kufanya mazoezi na kufuata mtindo bora wa maisha, kwani kuna ongezeko kubwa la wagonjwa, huku asilimia kubwa ya waathirika wakiwa ni wanawake.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani kwaniaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu, Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dk. Rashid Mfaume, amesema hadi kufikia mwaka 2030 athari za saratani zitakua mara mbili zaidi hasa katika nchi zenye kipato cha chini.

Pia amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa aliyoufanya katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), ambapo ametoa zaidi ya shilingi bilioni 18 za ununuzi wa vifaa tiba.

Alisema kutokana na uwekezaji mkubwa uliyofanyika kuna wagonjwa kutoka Zambia, Comoro , Msumbiji , Burundi na Kenya ambao wanafika ORCI kupata matibabu.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk. Julius Mwaisalage, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa anaoendelea kuufanya katika taasisi hiyo, ikiwemo ununuzi wa mashine ya kisasa ya uchunguzi wa saratani.

Alisema saratani inayoongoza ni ya Mlango wa kizazi inafuatiwa na saratani ya matiti.

Dk. Mwaisalage amesema ORCI inaendelea kusimamia utoaji huduma za kibingwa kuanzia kinga na uchunguzi huku akisema, maadhimisho ya siku ya saratani mwaka huu yana kauli mbiu isemayo ‘Saratani inatibika huduma sawa kwa wote’.

Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. Alphoncia Nanai, amesema katika kipindi cha mwaka 2022 kwa ukanda wa Afrika wagonjwa wa saratani walikua ni zaidi ya 800,000, huku takribani 600,000 wakipoteza maisha.

Shughuli hii imeambatana na uzinduzi wa mchezo wa Afya game ambapo kwa shilingi 500 tu utachangia mgonjwa wa Saratani huku ukijiweka katika nafasi ya kushinda pikipiki, Nyumba na simu kibao, mchezo huu umeandaliwa na wamata kwa udhamini wa Infinix