WAZIRI WA AFYA, MHE. UMMY MWALIMU AMEAGIZA TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD (ORIC) KUANZA KUTOA MATIBABU YA PET -CT SCAN

      Comments Off on

WAZIRI WA AFYA, MHE. UMMY MWALIMU AMEAGIZA TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD (ORIC) KUANZA KUTOA MATIBABU YA PET -CT SCAN

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORIC) kuanza kutoa matibabu ya PET -CT Scan ifikapo Februari Mosi Mwaka huu, kutokana na kukamilisha kwa jengo la kutoa huduma hiyo na kufungiwa mashine hiyo ya mionzi, kwani sababu kubwa ya wagonjwa wengi wa saratani kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Waziri Ummy aliyasema hayo mapema leo alipofanya ziara hapa Taasisi ya Saratani Ocean Road na kukagua jengo jipya litalotumika kutoa huduma za mionzi ikiwemo PET CT, pamoja na Cyclotron.

Aidha waziri Ummy Alisema kuwa wataendelea kuboresha huduma zaidi hususan kujenga wodi nzuri zenye ubora, kuhakikisha wanawavutia watu wa viwango tofauti vya maisha kuja kutibiwa nchini.

Waziri Ummy alisema serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika Taasisi hiyo, kuhakikisha inaboresha huduma zake na miundombinu, ili watanzani wapate huduma bora za matibabu ya saratani.

Kuhusu kuanza kwa mashine ya PET CT Scan, aliwataka kuhakikisha wanaanza huduma hizo za matibabu haraka kutokana na kukamilika miundombinu ya kutolea huduma, ambapo atawaomba kiongozi mmoja kuizindua ili kuanza rasmi kutoa huduma kwani ndio sababu kubwa ya wagonjwa hao kwenda nje ya nchi.

Katika hatua nyingine waziri Ummy aliagiza ORCI, kuhakikisha wanaanza kutoa huduma za upasuaji wa saratani ili kuwaepushia usumbufu wagonjwa kuzunguka katika hospitali zingine, wakati wangependa kutibiwa hospitalini hapo na kumaliza kila kitu.

“Mmenambia kila kitu mnacho, chumba kipo mtaalamu mnaye, hivyo hadi kufika Julai Mosi, muwe mmeanza kutoa huduma hii, mana hiyo itakuwa inaakisi dhamira nzima ya Taasisi hii ya saratani na umahiri wake wa kuwa kituo bora cha umahiri wa kutibu saratani na kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali hususani katika mashine za mionzi,” alisema

Alisisitiza kuwa, serikali itaendelea kusikiliza Taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo hivyo na wao wahakikishe wanatanua utoaji wa huduma na kuwajengea uwezo wataalamu katika hospitali za Kanda na mikoa.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy, ameipongeza Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa utoaji huduma bora zilizopunguza malalamiko kwa wananchi na kusaidia Watanzania wengi kupitia huduma zinazopatikana katika hospitalini hapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Julius Mwaiselage alimshukuru Waziri Ummy kufanya ziara katika taasisi hiyo huku akimpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea fedha za ujenzi wa miundombinu.

Alisema kwasasa wanayo mipango mbalimbali ya kujenga jengo jipya katika eneo la tasisi hiyo, huku wakiendelea na mipango ya kuandaa michoro ya ujenzi wa majengo ya kutoa matibabu ya saratani Dodoma na Mbeya.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dk.Mark Mseti alisema wataendelea kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi ikiwemo kutoa msamaha kwa wagonjwa wasio na uwezo.