“Tiba shufaa kuingizwa katika mtaala wa mafunzo ya afya nchini”, hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za utengemao, Tiba shufaa na wazee kutoka wizara ya afya Dkt. Mwinyikondo Amir kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama katika maadhimisho ya siku ya Tiba shufaa Duniani.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa afya nchini.
Dkt. Mwinyikondo kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mhagama amesema wizara ya afya ipo katika mchakato maalum wa kuingiza Tiba shufaa katika mtaala wa mafunzo ya afya nchini.
Ameendelea kusema serikali inawashukuru wadau mbalimbali wa Tiba shufaa nchini kwa kuwapa mafunzo watumishi wa afya ili kuongeza wataalamu wa Tiba shufaa nchini.
Tiba shufaa hutolewa kwa ushirikiano shirikishi wa wataalamu wenye taaluma mbalimbali wakiwemo madaktari, wafamasia, wauguzi, maafisa ustawi wa jamii pia wataalamu wa saikolojia, wataalamu wa magonjwa ya akili, wataalamu wa lishe, viongozi wa dini na wengine kutokana na uhitaji wa mgonjwa.
Dkt. Mwinyikondo ameipongeza Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa kuanza kuwatembelea wagonjwa na kuwapelekea huduma pale walipo hasa majumbani.
Huduma hiyo ya majumbani ni kitendo ambacho itasaidia sana kupunguza idadi ya wagonjwa mahospitalini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Julius Mwaiselage amesema karibia asilimia themanini ya wagonjwa wa Saratani wanaitaji huduma ya Tiba shufaa.
Na Taasisi ya Saratani Ocean Road imejikita katika kuimarisha huduma za Tiba shufaa zinazotolewa katika Taasisi na majumbani.
Pamoja na hayo Dkt. Mwaiselage amesema upatikanaji wa dawa ya Morphine ni asilimia miamoja zinapatika katika Taasisi.