MAADHIMISHO YA SIKU YA MASHUJAA WA SARATANI

      Comments Off on

MAADHIMISHO YA SIKU YA MASHUJAA WA SARATANI

Wito umetolewa kuongeza nguvu katika kuelimisha jamii ili kuongeza mashujaa wa Saratani na kuleta matumaini zaidi kwa wagonjwa.

Akizungumza na mashujaa pamoja na wadau mbalimbali wa Afya katika maadhimisho ya siku ya mashujaa Duniani leo tarehe 2 Juni 2024, Mkurugenzi msaidizi wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka wizara ya Afya Dkt. Omari ubuguyu ambae pia ndie aliyekuwa mgeni Rasmi amesisitiza kuwekeza kwenye utoaji wa elimu kwani ndio njia pekee itakayosaidia kupunguza kasi ya ugonjwa huu.

Aidha Dkt. Ubuguyu amesema kuwa Sera ya afya ina vipengele vya kutoa misamaha kwa wagonjwa wasio na uwezo na serikali inafanya hivyo kupitia Taasisi zake kama hii Taasisi ya Saratani Ocean Road husamehe pia ingawa amesisitiza kuwa kwa wale wenye uwezo inabidi wachangie ili kufanya shughuli ya utoaji huduma kuwa nyepesi na kuongeza wigo wa kusaidia watu wengi zaidi wasio na uwezo.

Nae Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt Julius Mwaiselage amesema kuwa kwasasa huwa wanatoa misamaha hadi Bilioni mbili kwa mwezi lengo likiwa ni kila atakaefika katika Taasisi hii awe na uwezo au hata asiwe na uwezo, apate huduma ya matibabu.

Katika hatua nyingine Dkt. Mwaiselage ameihabarisha jamii kuwa ufungwaji wa mashine ya PET-CT Scan upo tayari na matumizi yake yataanza mapema mwezi huu wa sita kwani tayari majaribio ya matumizi yake yamekwishafanyika na kufanikiwa kwa asilimia Mia moja.

Dkt. Mwaiselage amesema huduma ya upasuaji kwa sasa itakuwa ikifanyika hapa hapa katika Taasisi hii kuanzia mwezi wa nane mwaka huu wa 2024, kwani marekebisho madogo madogo yanaendelea.

Dkt. Mwaiselage amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupatikana kwa mashine stahiki pamoja na ujenzi na ukarabati wa majengo kwaajili ya huduma hizo.

Nae mkurugenzi wa Shujaa Cancer Foundation Bi Gloria Kida amewashukuru Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwao kwenye maandalizi ya shughuli hii.