WAJUMBE WA KAMATI YA UTEKELEZAJI WILAYA,JUMUIYA YA WAZAZI WA CCM IKIONGOZWA NA MWENYEKITI WA TAASISI YA MWALIMU NYERERE FOUNDATION WAMEFANYA ZIARA MAALUM KATIKA TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD

      Comments Off on

WAJUMBE WA KAMATI YA UTEKELEZAJI WILAYA,JUMUIYA YA WAZAZI WA CCM IKIONGOZWA NA MWENYEKITI WA TAASISI YA MWALIMU NYERERE FOUNDATION WAMEFANYA ZIARA MAALUM KATIKA TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD

Wajumbe wa kamati ya utekelezaji wilaya, jumuiya ya wazazi wa chama Cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Ilala ikiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation Mhe. Joseph. W. Butiku Leo mapema wamefanya ziara maalum katika Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Katika ziara hiyo Mh. Butiku ameshiriki na viongozi wengine wa Jumuiya ya wazazi wa CCM na Taasisi ya Saratani katika kupanda miti ya kivuli katika maeneo ya Taasisi ya Saratani.

Jumuiya ya wazazi wilaya ya Ilala imefanya ziara hiyo katika kuadhimisha wiki ya wazazi kitaifa.

Aidha Mhe. Butiku ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa kazi nzuri zinazofanyika katika kuwahudumia wagonjwa.
Mhe. Butiku ameendelea kusema kuwa kazi inayofanywa na Serikali katika kujenga majengo, huduma, ununuzi wa vifaa pamoja na madawa, hayo yote ni katika kudumisha amani, kudumisha umoja na kuleta maendeleo ya watu wote.

Pamoja na hayo Mhe. Butiku amesema PET/CT Scan ndio yenyewe katika uchunguzi na sasa imekwisha fika katika Taasisi ya Saratani, tuipongeze serikali yetu kwa kuleta mashine hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Dkt. Julius Mwaiselage amesema Taasisi ya Saratani kupitia serikali ya Jamuhuri ya Tanzania inatekeleza miradi ya maendeleo kutokana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kutokana na uboreshaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali katika eneo la matibabu na uchunguzi wa kibingwa na ubingwa bobezi, Rufaa za matibabu nje ya nchi zimepungua. Na itakapokamilika kwa usimikaji wa PET/CT Scan pia itasaidia wale wagonjwa wa Rufaa kwa ajili ya mashine hiyo kupata huduma hizo hapa hapa nchini amesema Dkt. Mwaiselage.

Aidha Dkt. Mwaiselage amesema kuwa Taasisi kwa hivi sasa ina mashine nne za Tiba Mionzi. Na kwa hivi sasa wagonjwa ni wengi wenye mahitaji ya tiba mionzi.

Hivyo Taasisi inahitaji kuongeza mashine nyingine nne ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa kwa ufanisi wa hali ya juu kabisa.

Pamoja na hayo Dkt. Mwaiselage ameishukuru jumuiya ya wazazi kwa kufanya ziara katika Taasisi ya Saratani na kutoa ahadi ya kusimamia miti kwa kuitunza miti hiyo iliyopandwa.