TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD LEO IMEPOKEA MSAADA WENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 137 KUTOKA KWA KAMPUNI YA GSM

      Comments Off on

TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD LEO IMEPOKEA MSAADA WENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 137 KUTOKA KWA KAMPUNI YA GSM

Taasisi ya Saratani Ocean Road leo imepokea msaada wenye thamani ya Shilingi milioni 137 kutoka kwa mmiliki wa kampuni za GSM Bw. Ghalib Said Mohamed katika kusheherekea siku yake ya kuzaliwa, ambapo pamoja na msaada huo ameshiriki chakula na watumishi wa Taasisi hiyo pamoja na wagonjwa.

Katika sherehe hiyo ambayo imefanyika katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Albert Chalamila ndiye alikuwa mgeni rasmi ambapo ametoa wito kwa watanzania kutoa sadaka ili kuwasaidia wagonjwa katika mahitaji yao ya matibabu kama ambavyo amefanya leo Bw. Gharib Mohamed.

Aidha Mh. Chalamila amesema kuwa watanzania hatuna budi kumshukuru Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mashine mbalimbali katika Taasisi hii ikiwemo Pet CT-Scan ambayo itaweza kuchunguza Saratani katika hatua ambazo mashine nyingine hazitaweza huku akisisitiza kuwa muda si mrefu itaanza kufanya kazi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage amemshukuru mmiliki wa GSM kwa msaada wake aliotoa wa vifaa hivyo.

Dkt. Mwaiselage amesema vifaa hivyo ikiwemo vile vya Tiba ya Saratani vitasaidia katika huduma mbalimbali kwa wagonjwa wa Taasisi hiyo, huku vikirahisisha utoaji wa huduma hizo kwa jamii ya watanzania na wanaotoka nje ya mipaka ya Tanzania.