ZIARA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII.
ZIARA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII.
ZIARA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII.
Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti Mhe. Stanslaus Nyongo ilifanya ziara tarehe 15/03/2021 kutembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Taasisi zilizoidhinishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan mradi wa ununuzi wa Mashine ya kisasa ya teknolojia ya nuclear medicine ya kupima saratani mwilini “Positron Emission Tomography Computerized Tomography scan (PET/CT scan)”.


Cyclotron
Ziara ya kamati hiyo ilianza kwa waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Nyongo pamoja na Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Dkt Dorothy Gwajima aliyeambatana na naibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt Godwin Mollel kukaribishwa katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, ambapo baada ya Risala ya Mwenyekiti wa Kamati na Utambulisho wa Washiriki, iliwasilishwa Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi na Mradi wa PET/CT Scan na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Mkurugenzi Mtendaji aliielezea kamati juu ya historia ya mradi huu uliopendekezwa mwaka 2016/2017, umuhimu wa mradi kwa taifa na utendaji kazi wa mashine. Mkurugenzi mtendaji alieleza kuwa “Mashine hii inahitaji mgonjwa kuwekewa dawa za nyuklia kupitia mshipa wa damu na mgonjwa kuingizwa katika mashine ya PET/CT scan ili kupimwa na kuangalia ugonjwa ulivyoenea mwilini na kuwa pia mradi unahusisha ujenzi wa Jengo la kusimika mashine husika, na vyumba vya kuweka dawa za nyuklia kwa mgonjwa na mradi unahusisha ununuzi wa mashine ya Cyclotron. Hii ni mashine ambayo inazalisha dawa za nyuklia (radioisotopes) ambazo mgonjwa atapatiwa.

Baada ya wasilisho la taarifa ya utekelezaji, kamati ya bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii, ilifanya ziara kutembelea Kutembelea Taasisi na hasahasa kuangalia eneo lililotengwa kwa ajili ya Mradi wa PET/CT scan, kuangalia Huduma za Tiba Mionzi za LINAC na kuangalia Huduma za Nuclear Medicine.







Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii kwa niba ya wajumbe, aliipongeza sana Serikali ya awamu ya tano na Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa uwekezaji na utekelezaji makini uliozingatia sheria za manunuzi na mikataba. Mwenyekiti alisema kuwa uwekezaji huo wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha kufanya vipimo vya Saratani kwa kutumia PET Scan na ujenzi wa kiwanda cha kuzalishia mionzi dawa ya radio isotopes itaifanya nchi ya Tanzania kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa kimatibabu.

Akielezea kuhusiana na mradi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima alisema, “Serikali inafanya mapinduzi makubwa na makini katika kuhakikisha kuwa ubora wa huduma za afya kwa watu wote zinaimarishwa na kutolewa kwa wakati na ufanisi. Na kwa kuwa magonjwa yasiyoambukiza yana njia za kuzuia ikiwamo kufanya mazoezi, basi amewashajihisha watanzania kujua njia za kujikinga na kufanya mazoezi kwa wingi.

Usiache uchunguzi wa awali wa saratani ya kizazi ata kama umeacha kujamiana
Usiache uchunguzi wa awali wa saratani ya kizazi ata kama umeacha kujamiana
Waliohudhuria mafunzo uchunguzi saratani ya kizazi Tanga, wanena
Waliohudhuria mafunzo uchunguzi saratani ya kizazi Tanga, wanena
Kambi ya uchunguzi wa saratani ya kizazi yaanza mkoani Tanga, Wanawake 1000 kuchunguzwa
Kambi ya uchunguzi wa saratani ya kizazi yaanza mkoani Tanga, Wanawake 1000 kuchunguzwa
Kambi maalum ya kampeni ya uchunguzi na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa Mkoa wa Tanga, imeanza rasmi leo Januari 28, 2021 ikitarajiwa kukamilika Januari 30, 2021, Wanawake wapatao 1,000 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi na wataalamu mabingwa wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).


Mabingwa hao wa ORCI wamepiga kambi hiyo wakishirikiana na Wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, ambapo awali walianza kwa kuwapa mafunzo wahudumu wa afya katika kufanya uchunguzi wa awali saratani ya mlango wa kizazi na matibabu.
“Tunawajengea uwezo watoa huduma Mkoa wa Tanga, Halmashauri na Wilaya zote za mkoa huu, washiriki waliohudhuria mafunzo haya ni zaidi ya 25, tunawakaribisha wakazi wa Tanga kutumia fursa hii ambapo tutakuwa hapa kwa ajili ya kuwahudumia,” amebainisha Dk. Kahesa

Ameongeza “Saratani ya kizazi inashika namba moja kwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudumiwa Ocean Road, Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa 10 ambako watu wameathirika na saratani hii, kwa hiyo program hii itasaidia kuibua wale wenye matatizo mapema, watapata matibabu mapema na hivyo tutaweza kujenga afya kwa kina mama

Amesema ingawa walengwa wakubwa wa kampeni hiyo ni wanawake, hata hivyo wanaume hawajaachwa nyuma na kwamba wale watakaofika hospitalini hapo watapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya tezidume, wasisite kujitokeza.
Akizungumza, Mkazi wa Tanga Mjini Jafari Ali amepongeza ushirikiano huo wa wataalamu wa Ocean Road na wenzao wa Mkoa wa Tanga kwa kufanya kampeni hiyo kwani imemuwezesha naye kupata fursa ya kufanya uchunguzi wa saratani ya tezidume.
“Niliona matangazo yaliyobandikwa, nikaamua kufika, nimepata vipimo wala hakuna tabu, nimechunguzwa kwa kipimo cha damu, leo tarehe 28 ni siku ya kwanza, 29 na 30 wataalamu watakuwa hapa Bombo, wanaume wenzangu wajitokeze na wanawake pia wafike kuchunguzwa saratani ya kizazi,” ametoa rai

Mkazi wa Wilaya ya Mkinga, Asia Hussein Ngoma amewasihi wakazi wenzake wa Tanga kuchangamkia fursa hiyo ya huduma ya uchunguzi na matibabu ya awali kwa saratani ya kizazi inayotolewa na wataalamu hao.
“Kule ninapoishi mimi ni kijijini, nilisikia matangazo redioni, nikafunga safari kuja hapa, nimekuonwa na madaktari, wamenichukua vipimo vizuri, wamenihudumia vizuri, nawasihi na wenzangu waje, waonwe na wataalamu hawa wenye lugha nzuri, huduma nzuri, wahudumiwe, wafarijike,” ametoa rai
Waziri Gwajima apongeza uboreshwaji wa huduma na upatikanaji wa dawa za saratani akiwa ziarani ORCI
Waziri Gwajima apongeza uboreshwaji wa huduma na upatikanaji wa dawa za saratani akiwa ziarani ORCI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima akiwa ziara ya kikazi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), amepongeza jitihada kubwa za uboreshwaji wa huduma na upatikanaji wa dawa za kutibu saratani uliokua kutoka asilimia 4 mwaka wa fedha 2014/2015 na kufikia asilimia 96 kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika ziara ya kikazi ORCI, amesema kuwa lengo lake ni kujionea hali ya utoaji wa huduma, changamoto na mwelekeo kwa ujumla pamoja na kuwapongeza na kuwatakia utekelezaji mwema wa ilani ya chama tawala katika awamu ya tano wataalamu wote wa afya nchini hususani mabingwa katika ngazi zote.

Mheshimiwa Waziri Dkt. Dorothy amesifu hatua zinazochukuliwa na Taasisi ya saratani katika kupunguza idadi ya rufaa za nje ya nchi kutokana na huduma hizo kupatikana hapa nchini, pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa mataifa ya nchi jirani wanaofika na kutibiwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, amesema, azma ya Serikali ni kuzifanya Taasisi zetu ziwe na uwezo wa kipekee wa kutoa huduma bora zinazoweza kuwavuta raia wa mataifa makubwa kuja kutibiwa katika mahospitali yetu nchini. Pia, amesifu kwa Kiasi kikubwa utekelezaji wa ilani ya chama tawala kwa kusaidia idadi kubwa ya wananchi wasio na uwezo wa kulipia matibabu ya saratani kwa kutoa misamaha ya dawa na matibabu. Misamaha kwa wanufaika iliyotolewa na Taasisi iliongezeka kutoka wanufaika 194,470 mwaka 2015/16 hadi kufikia wanufaika 495,538 mwaka 2019/20

Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage awali ya yote, alimkaribisha Waziri Gwajima, na kumpongeza kwa kuteuliwa kwake kuwa mbunge na kisha kuwa Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ambapo alimuahidi kuwa ORCI itashirikiana naye kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali na ilani ya Chama Tawala yanatekelezwa kwa ufanisi.

Mkurugenzi Dkt. Mwaiselage alielezea mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoikabili Taasisi ya Saratani pamoja na mikakati inayofanywa kukabili changamoto hizo. Ambapo, alimuomba Mheshimiwa Waziri kusaidia katika utatuzi wa changamoto ambazo upo katika ngazi ya Wizara ikiwamo utozwaji wa kodi wa vipuri vya vifaa tiba vinapoingizwa nchini kwa ajili ya kutengeneza vifaa tiba na pia ucheleweshwaji wa utoaji wa dawa na vifaa tiba hivyo


Mheshimiwa Waziri Dkt. Dorothy Gwajima akiwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road wakitembelea kuangalia utendaji kazi wa duka la dawa OCP.







Maelfu wafika ofisi za Efm & TV E kuchunguzwa saratani ya matiti
Maelfu wafika ofisi za Efm & TV E kuchunguzwa saratani ya matiti
Mwamko wa wananchi kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti unazidi kuongezeka kwenye jamii hadi kwa kundi la wanaume.

Leo katika Ofisi za Efm na TV E zaidi ya watu 1,000 wamejitokeza kuchunguza afya zao ambapo kati ya hao wanaume ni zaidi ya 100.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa, amesema hiyo inaonesha wazi kwamba elimu juu ya magonjwa ya saratani inazidi kufika kwenye jamii.

Amesema saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaowaona na kuwatibu Ocean Road na kwamba kwa mwaka takriban wagonjwa 800 huwa ni wenye saratani ya matiti.
“Mwezi Oktoba, kila mwaka duniani ni mahususi kwa ajili ya uelimishaji na uchunguzi wa saratani ya matiti, ili kuweza kuwagundua na kuwatibu mapema wagonjwa.
“Ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha, ORCI tumeshirikiana na Efm na TV E katika kuhitimisha kampeni ambayo tumeifanya mwezi mzima. Kampeni hii imetutia moyo, tunashukuru vyombo vya habari vimetusaidia…
“Si kitu cha kawaida kina baba kujitokeza kwa wingi namna hii hasa maeneo ya mijini ikizingatiwa pia ni mwisho wa wiki, hapa tumeweka vituo sita vya kufanya uchunguzi wa awali, vifaa na wataalamu tupo,” amesema.

Ameongeza “Tunapenda kuhamasisha jamii washiriki uchunguzi wa awali ni bure kwa wale ambao hawatapata fursa kushiriki hapa leo, tunawakaribisha kufika ORCI kule tunaendelea kutoa huduma hii kila siku.
Dk. Kahesa ambaye pia ni Mbobezi wa Magonjwa ya Saratani amesema huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti zinapatikana nchi nzima ambapo Serikali imeweka mtandao wa vituo zaidi ya 700.
“Ocean Road ina wabobezi na vifaa vingi na huwa tunafanya huduma hizi za mkoba tunaifikia jamii kwenye makazi yao, tunatoa elimu kuhusu visababishi vinavyoweza kuongeza hatari ya mtu kupata saratani, tunahamasisha Jamii kujenga tabia ya kuchunguza mara kwa mara.
“Kwa sababu inaweza kugundua mapema na inapogundulika mapema inatibika na mtu kupona kabisa, sasa hivi Tanzania tunao mashujaa waliotibiwa na kupona baada ya miaka 20,” amebainisha.
Naye, Daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Kandali Samwel, amesema ingawa tafiti zinaonesha wanawake ndiyo huathiriwa zaidi na saratani ya matiti, inapowaathiri wanaume huwa kali kidogo.
“Kitaalamu tunasema inakuwa addresive’ yaani inasambaa kwa haraka zaidi kuliko kwa wanawake, kwa sababu
mwenendo wa matibabu yao huwa tofauti na wanawake,” amesema.
Ameongeza “Hamasa kubwa tunayosisitiza ni watu kuchunguza mapema ili kuokoa maisha, kwani ikigundulika mapema inatibika na kupona kuliko mtu anapochelewa.
“Changamoto kubwa tunayoiona kwenye Taasisi yetu ni watu kufika wakiwa wamechelewa na ugonjwa ukiwa upo katika hatua za juu,” amesema Dk. Kandali.
Meneja Mkuu wa Efm na TV E, Mohamed Lukwili amesema huo ni mwanzo wa ushirikiano kati yao na Ocean Road katika kuifikia jamii.
“Tulianza ushirikiano baada ya sisi wafanyakazi wa Efm na TV E kwenda Ocean Road, kufanyiwa uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani, tukaona isiishie pale kwa sababu vyombo vya habari vinatazamwa kama muhimili wa nne kwenye nchi yetu, tunasikilizwa na wengi, maana yake tuna nafasi kubwa kushawishi watu wafahamu hali zao.
“Hivyo, leo tumewakusanya wanaume kwa wanawake ili wapate nafasi ya kupima saratani ya matiti na tezidume kwa wanaume, tangu saa mbili asubuhi hadi kufikia saa tisa jioni, tumeandikisha watu wapatao 1,400, lengo letu ni kuwezesha wengi zaidi wafanya uchunguzi hata wakifika 2,000 tutawahudumia.
“Kwa sababu tunafahamu saratani ni ugonjwa unaotesa ndugu zetu wengi Tanzania, tunapopata wananchi wengi zaidi inamaanisha waligundulika mapema tutakuwa tumeokoa wengi zaidi,” amesema.
Ameongeza “Mwamko ni mkubwa wamefika hata wenye umri wa miaka chini ya 18 jamii imeelimika kwamba magonjwa haya si tu yanatesa wazee bali hata watu wa rika nyinginezo wanaathirika.
Wanachuo zaidi ya 200 Veta (ICT – Kipawa) wafikishiwa elimu saratani ya matiti
Wanachuo zaidi ya 200 Veta (ICT – Kipawa) wafikishiwa elimu saratani ya matiti

Wanachuo zaidi ya 200 wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta (ICT- Kipawa wamepewa elimu sahihi kuhusu saratani ya matiti, jinsi ya kujikinga, uchunguzi na matibabu.
Elimu hiyo imetolewa leo na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), waliofika chuoni hapo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha mwezi wa Oktoba ambao kidunia ni maalum kwa ajili ya uelimishaji kuhusu saratani hiyo.

Akizungumza na wanachuo hao, Daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Kandali Samwel amewahimiza kuepuka visababishi vinavyoweza kuwapelekea kupata saratani hiyo ikiwamo mtindo usiofaa wa maisha kama vile unywaji wa pombe na uvutaji sigara, kutokufanya mazoezi na matumizi ya vyakula vyenye chumvi na sukari kwa wingi.
“Saratani hii kwa asilimia 99 inawapata wanawake na kwa asilimia moja wanaume, ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kila mwaka kwa kuwaona wataalamu kujua iwapo umepata saratani hii au la, ili pia kugundulika mapema na kupatiwa matibabu mapema,” ametoa rai.
Ameongeza “Kwa sababu ikigundulika mapema inatibika, lakini mtu akichelewa matibabu yake huwa hayatoi matokeo chanya, zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanaokuja pale ocean road wamechelewa kugundulika.
Daktari huyo amewasihi wasichana kujiepusha na matumizi holela ya muda mrefu, pasipo kuzingatia ushauri wa daktari, kwa wingi kupita kiasi kwa vidonge vya dharura vya kuzuia mimba maarufu P2, kwani ni tabia hatarishi inayoonekana kuchangia kupata saratani hiyo.
“Pale Ocean Road miaka ya hivi karibuni tunagundua hadi wasichana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 25 wana saratani ya matiti, wapo wanaoeleza wametumia dawa hizo bila ushauri wa daktari, kwa wingi na kwa muda mrefu.
“Hata hapa chuo baadhi yenu wametueleza hivyo. Tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani zinaonesha watu wanaotumia holela, kwa wingi vichocheo hivyo wapo kwenye uwezekano mkubwa kuishia kupata saratani hiyo.
“Hivyo, tunapata hizo taarifa, tunatilia maanani na tunaendelea kutoa elimu sahihi ili mbeleni tusije tukapata shida, hii inatufumbua macho na huu ni wito kwa kwa upande wa tafiti tuangalie shida hii ipo kwa kiwango gani kwenye jamii.
“Sisi tunaona tu kama wahudumu watu wanatoa hizi shuhuda, lakini hatuwezi kujua kwa kiwango gani pengine tatizo ni kubwa zaidi, hili linaweza kuletewa majibu na tafiti za kisayansi zaidi.
“Kimsingi dawa hizi zinapaswa kutumiwa pale tu dharura inapotokea ndiyo maana zinaitwa ‘emergency contraceptive’, zimewekwa kwa ajili ya dharura na dharura kutokea labda ni mara moja, kwa mfano kwa mtu ambaye anaweza kujamiiana pasipo kutarajia kile kitendo labda amebakwa na sisi wataalamu tunatarajia kitendo hicho si cha mara kwa mara.
Amesema njia za uzazi wa mpango zina kiwango cha homoni ambazo zinakuwa zimepimwa kwa wakati huo, lakini kumbe jamii wanafanya kuwa matumizi ya mara kwa mara, kwa wingi bila ushauri wa wataalamu, wanameza kama karanga.
Amesema pamoja na hilo, vipo visababishi vingine vinavyoweza kuchangia mwanamke kupata saratani ya matiti ikiwamo kuchelewa kuzaa, kutokuzingatia kunyonyesha ipasavyo, kurithi kwenye familia na sababu nyinginezo.

Awali, Kaimu Meneja Rasilimali Watu Veta- ICT Kipawa, Upendo Abraham ameshukuru wataalamu wa ORCI kufika chuoni hapo na kuelimisha wanafunzi na watumishi wake kuhusu saratani hiyo.
“Kwa sababu asilimia moja ya wanaopata saratani hii ni wanaume na asilimia 99 ni wanawake, tuna vijana hapa tuliona wakielimishwa kuhusu visababishi vya saratani hii elimu hii, itawasaidia na wale watakaokutwa na tatizo watapata matibabu kwa wakati.
“Wanafunzi 124 na watumishi 24 wakiwamo wanaume wameonesha utayari wa kuchunguzwa, hapa chuo wanafunzi wetu wengi ni wanaume kwa asilimia 75,” amesema.
Naye Miss Utalii wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sarafina Sisse amesema elimu hiyo imetolewa kwa wakati sahihi kwa kundi sahihi hilo la vijana kwani itawasaidia kujitambua na kuwahi kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.

“Ni jambo zuri walilofanya na mimi jukumu langu kubwa ni kuhamasisha jamii kupitia elimu hii, wanafunzi watatoka na kwenda kuwafikishia wengine kwa upana zaidi,” amesisitiza.

Wanafunzi Christina Steven na Steven Danford wameomba wataalamu hao kuendelea kutoa elimu kwa jamii hususan mashuleni ili wapate elimu sahihi itakayowasaidia kuepukana na ugonjwa huo.
Pamoja na wanachuo hao, wataalamu wa Ocean Road awali walizungumza pia na walimu na watumishi wa Chuo hicho na kuwapatia elimu juu ya ugonjwa huo.
Tiba ya mionzi dhidi ya saratani si tanuru la moto
Tiba ya mionzi dhidi ya saratani si tanuru la moto
Tiba ya mionzi inayotolewa na wataalamu wa magonjwa ya saratani si tanuru la moto kama ambavyo baadhi ya watu kwenye jamii wamekuwa wakidhani na kusambaza taarifa hizo zisizo sahihi.
Daktari Mbobezi wa Tafiti za Saratani wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Kandali Samwel amesema hayo wakati wa alipokuwa akizungumza na walimu, wafanyakazi na wanachuo wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA (ICT- Kipawa.

“Tunaona baadhi ya wagonjwa tunaowahudumia kule Ocean Road, tukiwaeleza wanatakiwa kupata tiba mionzi wanakataa, unasikia mgonjwa anasema ni kule wanakoingizwa kwenye tanuru la moto, jamani si kweli kwamba tiba ya mionzi ni tanuru la moto,” amesema.
Amesema tiba mionzi dhidi ya saratani imehakikishwa ni salama na kwamba haina uwezo wa kuunguza mwili kama vile tanuru liwakavyo na kuunguza.
“Jamii ielewe, ni tiba sahihi iliyohakikishwa usalama wake na tiba hii si kwamba daktari mmoja anaamua kumtibu mgonjwa, kumchukua na kwenda kumuingiza katika chumba cha matibabu, hapana!.
“Daktari anapopendekeza, kuna jopo la wataalamu sita wanaosimamia matibabu hayo, ni wataalamu wa fani mbalimbali wanaojumuika katika kutoa tiba hiyo kwa kila mgonjwa mmoja.
“Kuna hesabu mahususi ambazo hupigwa, wanafanya ‘calculation’ kulingana na mgonjwa husika, si kila mgonjwa atapewa mionzi aina hiyo hiyo, wanaangalia ugonjwa upo sehemu gani, umefikia hatua gani na mambo mengine mengi,” amesisitiza.
Amesema jambo la muhimu kwa jamii kuzingatia ni kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kuweza kubaini iwapo wanakabiliwa na magonjwa ya saratani au la ili kugundua mapema na kupata matibabu mapema.
“Tunaona zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanaokuja kule Ocean Road wamechelewa matibabu, inafanya ugumu hata katika kuwapa matibabu, ugonjwa unakuta upo hatua za juu, tunahimiza kufanya uchunguzi wa awali mapema,” ametoa rai.
Amesema katika kuadhimisha mwezi wa Oktoba, ambao ni mahususi kwa uelimishaji kuhusu ugonjwa wa saratani ya matiti, waliona vema kwenda kuzungumza na walimu, wafanyakazi na wanachuo wa VETA ICT- Kipawa. “Tumewapa elimu sahihi, maana kuna taarifa nyingi zisizo sahihi kwenye jamii, sambamba na elimu pia tunafanya uchunguzi wa awali, wale tutakaowakuta na tatizo tuweze kuwapa matibabu mapema na wengine wajue jinsi ya kuendelea kujikinga wasipate maradhi haya,” amebainisha

Jamii yaaswa kutoshiriki kukatiza matibabu kwa wagonjwa wa saratani.
Jamii yaaswa kutoshiriki kukatiza matibabu kwa wagonjwa wa saratani.
Jamii imeaswa kuacha kuwakatizia matibabu wagonjwa wa saratani kwa lengo la kuwapeleka kwenye maombi, tiba za asili na waganga wa jadi kwani wanaweza kuwasababishia madhara makubwa zaidi ikiwemo kifo.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt Julius Mwaiselage katika mafunzo kwa mashujaa wa saratani ya matiti yaliyofanyika Taasisini hapo ambapo yanalenga kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya saratani na jinsi ya kujikinga ambapo mwezi oktoba umetengwa mahususi katika kutoa elimu ya saratani kwa jamii.
Dkt. Mwaiselage amewataka waganga wa tiba za asili na watu wa maombezi kutowazuia wagonjwa wa saratani kuendelea kuhudhuria matibabu yao hospitali na pale wanapowapa dawa kushauriana kwanza na Daktari ili ijulikane dawa wanazotoa zinatibu ugonjwa gani.
“Nitoe wito kwa hawa wanaotoa tiba mbadala iwe ni maombi au wanaotangaza kuwa wanadawa za kutibu saratani kuacha kabisa kuwazuia wagonjwa wa saratani kuendelea na matibabu ambayo wanapatiwa na Taasisi ya Ocean Road kwani wanatupa wakati mgumu wa kuwatibu wagonjwa kutokana na kurudi hospitali wakiwa katika hatua ya tatu na nne ambayo ni changamoto kwa mgonjwa kupona”Amesema Dkt Mwaiselage.
Aidha amesema kwa sasa serikali imeboresha huduma za Afya katika Taasisi hiyo ikiwemo upatikanaji wa dawa, na vifaa tiba ikiwemo mashine za kisasa ambapo wagonjwa wanaweza kupata matibabu na kupona kabisa

Ameongeza kuwa kwa sasa huduma ya kutibu saratani ya matiti ambayo inashika nafasi ya pili kwa asilimia 15 kati ya wagonjwa wa saratani elfu 42 kila mwaka inatibika kwa kukuondoa tu uvimbe bila kukata titi lote na kwa waliokatwa titi tayari kuna Madaktari walioenda kupatiwa mafunzo nchini China na wakirudi watawafanyia upasuaji wa kurudisha titi.
Aidha katika mafunzo hayo pia kutatolewa elimu ya jinsi ya kuishi na saratani ndani ya jamii ikiwemo kunyanyapaliwa haswa kwa wale wanaokatwa titi, imani potofu kuwa saratani haiponi na matangazo ya kwenye mitandao ya uwepo wa dawa za kutibu ugonjwa wa saratani kutokana na wagonjwa wa saratani kuchukua mda mrefu kupona kwa kuzingatia taratibu za hospitali.
Hata hivyo amesema huduma za matibabu ya saratani zimeboreshwa katika kipindi hiki cha awamu ya 5 ambapo kila mwaka bajeti ya zaidi ya shilingi Bilioni 7 hutengwa kwa ajili ya dawa za saratani na kusababisha wagonjwa wa saratani kuishi kwa muda mrefu.
Dkt Mwaiselage amesema katika kipindi hiki cha mwezi mmoja cha kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa wa saratani watatoa huduma ya uchunguzi wa saratani na elimu kwa wananchi ili wajichunguze wenyewe pamoja na kuwasisitiza kuwahi hospitali mapema pindi wanapoona dalili za ugonjwa wa saratani.
Sambamba na hayo amesema baada ya kuboresha kwa huduma za Afya katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 wamekuwa wakipokea wagonjwa elfu 55 kila mwaka tofauti na awali walipokuwa wanapokea wagonjwa elfu 33 huku wanaotibiwa na kupona ni asilimia 60 tofauti na awali walikuwa wanapona asilimia 20 tu.

Kwa upande wake Meneja Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani Dkt Maguha Stephen amesema sababu zinazochangia kuongezeka kwa saratani ya matiti ni pamoja na wanawake kutonyonyesha kwa muda mrefu, kuacha kunyonyesha kabla ya miaka 2, aina ya ulaji wa vyakula ikiwemo vile vya mafuta, kupata hedhi mapema na kurithi.
Dkt Maguha amesema ugonjwa wa saratani bado ni tishio Duniani ambapo kila mwaka hupatikana wagonjwa milioni 18 hivyo jamii inapaswa kujilinda dhidi ya ugonjwa wa saratani hususani ya matiti ambayo kwa kiasi kikubwa huadhiri wanawake kwa asilimia 99 na wanaume kwa asilimia 1 kwa kula vyakula vya mboga mboga, samaki kunyonyesha kwa wakati na kufanya uchunguzi wa saratani mara kwa mara.

Nao baadhi ya mashujaa wa saratani waliohudhuria katika mafunzo hayo akiwemo Halima Mwaipopo ambaye ametibiwa miaka 18 sasa kwa kukatwa titi lake amesema kwa sasa anajisikia kupona kabisa na hiyo inatokana na kuzingatia taratibu zote alizokuwa anaelekezwa na Daktari pamoja na kutokata tamaa licha ya unyanyapaa aliokuwa anaupata ndani ya jamii alijipa moyo na kumuomba Mungu.

Shujaa wa Saratani Nyakolema Silla amtoa wito kwa wagonjwa wa saratani kutokata tamaa na kuzingatia hatua zote za matibabu wanazoelekezwa na Daktari pamoja na kukubaliana na hali zao kwani itawasaidia kuishi na jamii bila kujali changamoto za kunyanyapaliwa
+255-2127597
