Ebeneza Women Group wawafariji wagonjwa waliolazwa Ocean Road
Kikundi cha kina-mama ‘Ebeneza Women Group’ kimewatembelea, kuwajulia hali na kuwafariji wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), iliyoko Mkoani hapa.
Mapema leo baadhi ya wanachama wa hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Beatrice Masolwa, wamekabidhi zawadi mbalimbali kwa wagonjwa hao.[15/10, 10:30] Bwana: Akizungumza, Masolwa ametaja baadhi ya zawadi hiyo ‘diapers’ za watu wazima, miswaki, dawa za meno, sabuni za kuoga na kufulia maji na nyinginezo. “Thamani ya vitu vyote tulivyonunua ni kiasi cha Sh. 500,000,” amebainisha.
Amesema wameguswa kufika hospitalinihapo kuwaona na kuwafariji wagonjwa kwani ni sehemu ya jamii.[15/10, 10:30] Bwana: Amehimiza jamii kujenga na kuendeleza utamaduni wa kuwatembelea, kuwajulia hali na kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitalini. “Unapoishi jua kuna mgonjwa aliyelazwa hana ndugu, anahitaji msaada na faraja, sisi ndio wa kwenda, kuwafariji na kuwasaidia chochote tulichojaliwa,” ametoa rai Masolwa.[15/10, 10:30] Bwana: Wanahitaji upendo hasa wakati ambapo wapo wodini wakipatiwa matibabu na wakiendelea kupigania uhai wao,” amesisitiza. Ameongeza kwamba “Kuna watu wanahitaji kutiwa moyo na sisi tumeona ni watu wenye dhamana hiyo, tukaja kuwatembelea.
Na Mwandishi Maalum (ORCI) – Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road {ORCI}, Dk. Julius Mwaiselage amekemea tabia ya baadhi ya wanajamii kuwanyanyapaa wagonjwa wa saratani hasa waliofanyiwa upasuaji wa kuondoa matiti ikiwa ni sehemu ya kufanikisha matibabu dhidi ya saratani hiyo. Amekemea tabia hiyo mapema leo alipokutana na wanawake wapatao 30, mashujaa wa saratani ya matiti {waliogundulika, kutibiwa na kupona na wale wanaoendelea na matibabu dhidi ya saratani hiyo}. Amekutana nao kwenye viunga vya Taasisi hiyo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Mwezi wa Saratani ya Matiti {Oktoba} unaobeba dhima ya kuelimisha jamii na kuhimiza uchunguzi wa mapema ili kupata matibabu mapema, ulimwenguni.
“Jamii ielewe kuondolewa titi mwanamke haimaanishi u-‘u-namke’ wake umebadilika, bado upo vile vile na maeneo mengi kama mwanamke anayefanya ataendelea kuyafanya bali ni kiungo hiki kimoja tu ambacho tumekiondoa,” amesema. Amesisitiza kwamba saratani ya matiti inaathiri pia wanaume ijapokuwa kwao ni kwa kiwango kidogo cha asilimia moja tu na wanawake walichukua asilimia 99. Amesema ndani ya taasisi hiyo saratani ya matiti inashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa baada ya saratani ya kizazi inayoshika nambari moja. “ORCI tumeanza kutoa matibabu ya saratani mbalimbali nchini tangu mwaka 1996, kufikia sasa saratani ya kizazi inaongoza kwa asilimia 35, kisha matiti kwa asilimia 15, ukijumlisha idadi yote hii ni karibu asilimia 50, saratani zinazoshambulia wanawake zinaongoza kwa idadi ya wagonjwa,” amedokeza. Dk. Mwaiselage amesisitiza mapambano dhidi ya saratani ya matiti yanahitaji msukumo zaidi kukizuia isizidi kushambulia jamii kwani takwimu za taasisi hiyo zinaonesha miaka 10 iliyopita ilikuwa inashika nafasi ya nne kwa idadi kubwa ya wagonjwa lakini sasa inashika nafasi ya pili. “Ni tatizo linaloongezeka, nawashukuru wadau mbalimbali wanaotusaidia kuhamasisha na kuelimisha jamii hasa mashujaa hawa wanahimiza wengine wajitokeze kufanya uchunguzi mapema ili wapate matibabu mapema wanapogundulika,” amesema. Ameongeza “Serikali imeongeza miundombinu kwenye tiba na Kinga pia elimu inatolewa ili wananchi waelewe dalili na watibiwe hatua za awali, huduma za uchunguzi pia zimeenea nchini. Amesema nchi nzima vituo zaidi ya 800 vinavyofanya uchunguzi wa saratani ya kizazi na matiti na kwamba upatikanaji wa dawa za kutibu saratani ni mkubwa na umeimarika ka kiwango cha asilimia 98 “Hospitali zetu za Kanda ikiwamo Bugando, KCMC, Mbeya {MZRH}, Benjamin Mkapa na nyingine za binafsi huduma za uchunguzi wa saratani zinafanyika na zimekuwa bora katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kufikia sasa,” amesisitiza. Ameongeza “… ni kuchunguza na kutibu mgonjwa, kubwa kumshukuru MUNGU sisi tunatibu yeye anaponesha kabisa
anatusaidia. Amesema pamoja na unyanyapaa changamoto nyingine inayowakabili wagonjwa hao ni imani potofu ambazo huwarudisha nyuma na baadhi yao kuacha kuzingatia matibabu. “Wengi hufika ugonjwa ukiwa katika hatua za juu mno, Tanzania tuna huduma ya kuondoa vivimbe vya saratani pasipo kuondoa titi lote lakini Kwa sababu wengi huchelewa ndiyo maana wanalazimika kuondolewa titi lote, ndiyo maana tunahimiza mtu awahi kufanya uchunguzi mapema kwani ikiwahiwa hatua za awali ni rahisi kutibila pasipo kuondoa titi lote,” amesema. “Hivyo, siku kama leo, tunakutana na kujadili ni njia bora zaidi katika kutatua, duniani saratani ya matiti inaongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa, ni muhimu kutoa elimu kwa jitihada mbalimbali na kwa kushirkiana katika kuzuia na kutibu vizuri zaidi,” amesisitiza. Mashujaa hao hii leo pia wamepatiwa zawadi mbalimbali ikiwamo kanga, pochi na taulo za kike na Klabu ya Lions pamoja na benki ya.. ikiwa ni sehemu ya kusherehekea na kuwapa faraja kwamba hawapo peke yao katika mapambano hayo.
Teknolojia: Vitanda vya kisasa vya umeme, matibabu kwa wagonjwa Ocean Road
Vitanda viwili vilivyoundwa kwa teknolojia ya kisasa, vikitumia nishati ya umeme, inayosaidia kurahisisha na kuchochea ufanisi wa matibabu kwa wagonjwa waliolazwa wodini, vimekabidhiwa kwa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI). Msaada huo umetolewa na Kampuni ya Gama Pharmaceutical {T} Limited kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Czech kupitia Ubalozi wake nchini. Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya msaada huo mapema hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage amesema umegharimu kiasi cha Dola 8000 ambazo ni wastani wa kati ya Sh. milioni 17. “Utaona ni gharama kubwa, ni vya kisasa sana, ukienda hospitali zozote za kisasa duniani utaona vitanda vya namna hii,” amesisitiza. Amesema kukabidhiwa kwa mashine hizo kunaifanya taasisi hiyo kuwa na jumla ya vitanda vinane vinavyotumia teknokojia ya kisasa. “Ni maalum kwa ajili ya kuhudumia wale wagonjwa wanaokuwa wanaumwa sana wodini, tuna vitanda 25, vingine vinatumia njia mbalimbali kwa nguvu ya kupandisha na kushusha. “Kupata vitanda hivi viwili vya kisasa leo inafanya tunakuwa na jumla ya vitanda vinane vya kisasa kati ya hivyo 25, kwa hiyo vinakuwa rahisi kwa mhudumu na mgonjwa mwenyewe. “… anaweza kushusha na kupandisha kulingana na hali atakayokuwa naye, kwa maana hiyo tuna uhitaji wa vitanda 17 vya kisasa vinavyotumia umeme,” amesema. Ameongeza “Nimeomba kampuni hii ya kitanzania ambayo imeshirikiana na serikali ya Czech itusaidie tupate vitanda vingine. Dk. Mwaiselage amebainisha kwamba idadi ya wagonjwa wa saratani nchini inazidi kuongezeka hivyo ni muhimu pia kuzidi kuimarisha huduma za matibabu. “Karibu asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa wa saratani nchini wanakuja hospitalini katika hatua za juu za ugonjwa, kama wakitibiwa wanakuwa katika hali ‘seriously’ au karibu wanahitaji huduma za namna hii,” amesema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Gama Pharmaceutical, Qutibal Salaheldeen Ahmed amesema kampuni hiyo imeridhishwa na mazingira rafiki ya uwekezaji nchini Tanzania na kwamba kampuni hiyo inajivunia kutoa msaada huo na ipo tayari kuendeleza ushirikiano.Balozi wa Czech – Tanzania, Martin Klepetko amesema nchi hiyo ipo tayari kuendeleza ushirikiano wake na Tanzania katika kuimarisha na kuboresha maeneo mbalimbali kwenye sekta ya afya. Balozi Dk. Abdalah Posi ameshukuru kwa msaada huo akisisitiza kwamba jambo hilo {ushirikiano huo} ni jema.
“Teknolojia inakua kwa kasi anapokuja mtu kuamua kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa mchango kwa vitu hivi , ni jambo jema, inasaidia kuboresha sekta ya afya na kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Posi.Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza cha Wizara hiyo, Dk. Omary Ubuguyu amebainisha kwamba uhitaji wa vitanda vya namna hiyo nchini bado ni mkubwa. “Hospitali zetu zote za rufaa za kanda na Taifa vina uhitaji wa vitanda vya namna hii katika maeneo tunayotoa huduma za dharura, ICU na kama hizi za saratani na mengineyo,” amesema. Dk. Ubuguyu amebainisha mahitaji ya jumla ya vitanda hivyo si chini ya 100 kwa nchi nzima. “Mahitaji yapo mengi, tunaenda hatua kwa hatua ocean road sasa imefikisha vitanda vinane, hili la msaada wa Gama na Czech sisi inatuamsha zaidi kwamba sasa tunaweza kununua moja kwa moja kutoka kwa mzalishaji na hili ndilo jambo la msingi tulilolifurahia,” amesema.
Saratani ya Ovari inavogharimu waliochelewa kuzaa, wanene kuondolewa kizazi
Ni saratani nadra kutokea duniani, mwanamke mwenye saratani hii {ovarian cancer} mara nyingi huchelewa kugundulika mapema na hata wale wachache wanaogundulika hukutwa ugonjwa umefikia kiwango cha juu, ngumu kutibika. Hali hiyo husababisha wengi wao kuishia kung’olewa kabisa mji wa mimba {uterus}kwani saratani hiyo hukutwa imesambaa na kuathiri kwa kiwango kikubwa. Wanawake ambao hawajazaa kabisa au wale waliochelewa mno kuzaa juu ya umri wa miaka 35 wanatajwa kwamba ndilo kundi lililopo kwenye hatari na uwezekano mkubwa wa kupata saratani hii.
MATUKIO NA MAISHA BLOG imefanya mahojiano haya maalum na madaktari bingwa wa magonjwa ya saratani katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, wanafafanua kwa undani kuhusu saratani hii… Kulingana na takwimu za Taasisi ya Saratani Ocean Road kumekuwa na ongezeko kidogo la wanawake wanaopokewa wakikabiliwa na saratani ya ovari, rekodi inaonesha katika mwaka 2006 kulikuwa na wanawake 21 kwa mwaka waliokuwa wanatibiwa kufikia mwaka 2014 idadi iliongezeka hadi wanawake 49. Idadi hiyo ni sawa pungufu ya asilimia moja ya wagonjwa wote ambao walionwa kwenye taasisi hiyo katika kipindi hicho cha miaka minane mfululizo na kwamba idadi inaonesha kila mwaka ni takribani wagonjwa wapya wa saratani hiyo ni wanawake 40 hadi 50 wanaofika kupatiwa matibabu ndani ya taasisi hiyo. “Pamoja na kwamba ni saratani nadra lakini ni ngumu kutibika, mtu anapogundulika kuwa nayo,” anasisitiza Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa ORCI, Emmanuel Lugina. Dk. Lugina anasema tathmini ya Ocean Road inaonesha wanawake wanaofika kupatiwa matibabu wengi ni watu wazima wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea. “Inaweza kurithiwa {yaani} ikiwa mama yako aliwahi kuugua upo kwenye hatari ya kupata, wenye unene kupita kiasi wapo hatarini kupata saratani hii, wengine ni wasomi, ambao wamechukua muda mrefu kwenye masomo hawajazaa au wamezaa mtoto mmoja. “Kadri unavyoongeza idadi ya watoto inakuwa kinga dhidi ya saratani ya mayai, lakini hatuwezi kumpangia, kuna masuala ya uchumi na mwenuyewe alivyopangilia, ila tafiti zinaonesha ukiwa na watoto wengi hatari ya kupata saratani hii inakuwa inapungua,” anabainisha.
Anasema asilimia kubwa ya wagonjwa wanaowatibu ni wanene, unene uliochangiwa na sababu mbalimbali kutokea, ikiwamo ulaji usiofaa, wanakula vyakula vyenye mafuta mengi ambavyo si mlo kamili na hawajishughulishi kwa mazoezi. “… Mwisho wa siku wanakuwa na uzito mkubwa, mafuta yanaongezeka mengi chini ya ngozi, haya mafuta yana uwezo wa kubadilisha zile homoni {eostrejeni na …. na kuathiri yale mayai,” anasema. Dk. Lugina anafafanua kwamba usipofanya mazoezi, ukala vyakula vya mafuta, unakuwa mnene na hivyo kuongeza mafuta chini ya ngozi. “… na mwili una namna ya kugeuza yale mafuta yakawa homoni za kike na baadae yana uwezo wa kuathiri zile ovari, unene uliozidi ni nchanzo kikubwa si tu cha saratani bali magonjwa mengine sugu. “Unachangia saratani nyingi pia kama ya utumbo mpana, tezidume, matiti kwa wanaume ni kutokana pia na unene,” anasisitiza Bingwa huyo.
MFUMO WA OVARI Ovari ni miongoni mwa jozi muhimu za viungo ndani ya mwili wa mwanamke kukamilisha mfumo wake wa uzazi, kimaumbile huwa zipo mbili, moja upande wa kulia na nyingine kushoto mwa mfuko wa uzazi {uterus}. Kutoka kwenye mfumo wa uzazi hadi kwenye ovary kuna mirija ya falopio ambayo hii ndiyo kiunganishi kikuu, ovari zenyewe huwa katika ‘kaviti’ ya pelviksi na hujishikiza kwenye ligamenti mbili. Ligamenti hizi ni tishu za kuunganisha zenye nyuzi na uwezo wa kupinda ambazo hushikilia viungo mbalimbali vilivyopo ndani ya mwili kadhalika kuunganisha mfupa mmoja na mwiline kwenye jointi. Kibaiolojia zina kazi mbalimbali kuu ikiwa kutengeneza mayai ya kike ya uzazi, kuzalisha homoni mbalimbali za kike ikiwamo estrogeni ambayo ina kazi muhimu ya kukuza na kukomaa kwa viungo vya uzazi, kurekebisha na kuwezesha mzunguko sahihi wa hedhi, kuwezesha tabia za kike mfano kuota maziwa na kutanuka nyonga nakadhalika. Aidha ina kazi ya kumpa mwanamke hisia za tendo la kujamiiana, huku homoni nyingine ya ‘projesteroni’ nayo ikizalishwa humo kwa ajili ya kufanya kazi ya kuandaa mfuko wa uzazi kumtunza mtoto akiwa tumboni mwa mama na hata kuzuia mimba isiharibike baada ya kuundwa. Zipo pia homoni nyinginezo ambazo huzalishwa katika vifuko vya ovari ikiwamo ile ya relaxin ambayo hufanya kazi ya kuongeza ulaini wa mifupa na misuli ya nyonga wakati wa ujauzito ili kusaidia mtoto atoke kirahisi wakati wa kujifungua. Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani Ocean Road, Dk. Crispin Kahesa anafafanua kwamba saratani hiyo inakadiriwa kuchukua asilimia 1.7 ya saratani zote duniani kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO). Anasema ni ngumu kugundua saratani ya ovari katika hatua za awali kwani huwa haioneshi dalili za wazi ambazo muhusika anaweza kuhisi kuna tatizo linalomkabili. “Walio wengi wanafika ikiwa imesambaa kwenye tumbo la uzazi, tumbo kubwa na sehemu ya mfuko wa uzazi,” anabainisha.
MABADILIKO YANAVYOANZA Kahesa ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani anasema yapo mabadiliko kadhaa ambayo muhusika huyapata na wengi huwa hawayatilii shaka kwamba huenda kuna kitu ambacho hakipo sawa mwilini mwao. “Kubwa ni kubadilisha mfumo wa chakula, kwa njia ya kwenda haja, labda ulizoea asubuhi unapata {‘choo’}, unakuta inabadilika. “Anaona tumbo limejaa, wengine anakuwa anacheua, inaambatana na maumivu ya tumbo, kupoteza hamu ya kula, kwa muonekano tumbo lake huwa kubwa. “Hasa kutokana na maji yanakuwa yapo eneo la tumbo, anajisikia mwili kuishiwa nguvu na kupoteza uzito kwa sababu hamu ya kula inakuwa imeisha”. “Dalili nyingine huwa zinatokana na kiwango ambacho ugonjwa umefikia, kama ni hatua za juu sana ugonjwa unaleta madhara kwenye ini kwa hiyo atakuwa na dalili zinazonesha ini au figo limefeli,” anasema.
USHAURI Dk. Kahesa anasema jambo jingine la muhimu wanaloshauri kuzingatiwa ni kina mama kupata mimba katika umri ambao usizidi miaka 35 ili kuweza kuepuka saratani hii . “Walio wengi mimba hatarishi ni zile zinaanzia miaka 35 na kuendelea, kama ilivyo mimba hatarishi kwenye umri mdogo, ni zile chini ya miaka 25, “Tunaamini ukamilifu wa mama ni miaka 25, hatari inaonekana kadri umri unavyoenda, mimba ya kwanza {35}huu ni umri mwafaka,” anashauri. Kuhusu matibabu, Dk. Kahesa anasema huhusisha pande mbili ikiwamo upasuaji wa kuondoa uvimbe ulipo au tiba ya dawa za kemia. “Wengi wapo hatua za juu hupatiwa tiba mchanganyiko au mojawapo kati ya hizo. Tiba nyingine zinahusiana na kuondoa kizazi. “… atakuwa na maumivu atahitaji dawa za kumsaidia kupunguza maumivu, atahitaji dawa za kumsaidia kumpa hamu ya chakula, atakuwa amedhoofu atahitaji tiba lishe,” anabainisha Dk. Kahesa.
Kikao cha pili cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road. Ukumbi wa Edema, Morogoro 04/06/2021
Wajumbe wa Baraza la tano la wafanyakazi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road walikutana na kufanya mkutano wa pili wa mwaka 2020/2021 katika ukumbi wa mkutano wa Edema mkoani Morogoro kwa ajili ya kupokea ripoti ya utekelezaji, muhtasari wa bajeti iliyopitishwa na kusomwa bungeni na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Dorothy Gwajima (mb) na mwenendo wa utoaji wa huduma za uchunguzi, tiba, kinga na tafiti.
Mapendekezo kutoka kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi yakiwemo uboreshaji wa utoaji wa elimu zaidi kwa umma kupitia redio, luninga, mitandao ya kijamii pamoja na kuwatembelea wahudumu wa afya mikoani na wilayani. Mafunzo haya yajumuishe pia wataalamu wa huduma anuai katika Taasisi wanaohudumia wagonjwa kama wakufunzi kutokana na ujuzi walioupata katika utoaji huduma. Mafunzo haya yatawezesha rufaa ambazo si muhimu kuratibiwa na kufanyiwa kazi kuanzia katika ngazi za wilaya. Pia iwezeshe hata wale wagonjwa wanaoruhusiwa kutoka Ocean Road kuweza kupatiwa huduma bora wawapo wilayani kwao na si kunyanyapaliwa.
Maboresho mengine yaliyopendekezwa kwa upande wa kitengo cha ufundi (estate) katika kuharakisha utekelezaji wa majukumu yao ya utoaji wa huduma za kiufundi kwa ubobezi na kiufanisi.
Ocean Road yaweka kambi siku sita, mafunzo na uchunguzi saratani ya kizazi – Tabora
Baadhi ya wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), iliyopo Jijini Dar es Salaam, wapo mkoani Tabora kwa kambi ya siku sita inayojumuisha mafunzo sambamba na uchunguzi wa awali wa saratani ya shingo ya kizazi.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani ORCI, Crispin Kahesa amesema kambi hiyo imedhaminiwa na Bank ya NBC.
“Timu ya Wataalamu kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road tumeweka kambi mkoani Tabora kuanzia Juni 24 hadi 29, 2021. Tunatoa mafunzo ya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi,” amebainisha Kahesa ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani ORCI.
Amesema jumla ya watoa huduma wa afya 21 kutoka hospital, ‘dispensary’ na vituo vya afya vya Mkoa wa Tabora watanufaika na mafunzo kupitia kambi hiyo.
Ameongeza “Huduma ya uchunguzi wa awali wa saratani ya kizazi inafanyika bila malipo kwa wananchi wote
ZIARA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII.
ZIARA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII.
Kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti Mhe. Stanslaus Nyongo ilifanya ziara tarehe 15/03/2021 kutembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Taasisi zilizoidhinishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan mradi wa ununuzi wa Mashine ya kisasa ya teknolojia ya nuclear medicine ya kupima saratani mwilini “Positron Emission Tomography Computerized Tomography scan (PET/CT scan)”.
Cyclotron
Ziara ya kamati hiyo ilianza kwa waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Nyongo pamoja na Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Dkt Dorothy Gwajima aliyeambatana na naibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mheshimiwa Dkt Godwin Mollel kukaribishwa katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, ambapo baada ya Risala ya Mwenyekiti wa Kamati na Utambulisho wa Washiriki, iliwasilishwa Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi na Mradi wa PET/CT Scan na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kudumu Mheshimiwa Stanslaus Nyongo (Mb)
Mkurugenzi Mtendaji aliielezea kamati juu ya historia ya mradi huu uliopendekezwa mwaka 2016/2017, umuhimu wa mradi kwa taifa na utendaji kazi wa mashine. Mkurugenzi mtendaji alieleza kuwa “Mashine hii inahitaji mgonjwa kuwekewa dawa za nyuklia kupitia mshipa wa damu na mgonjwa kuingizwa katika mashine ya PET/CT scan ili kupimwa na kuangalia ugonjwa ulivyoenea mwilini na kuwa pia mradi unahusisha ujenzi wa Jengo la kusimika mashine husika, na vyumba vya kuweka dawa za nyuklia kwa mgonjwa na mradi unahusisha ununuzi wa mashine ya Cyclotron. Hii ni mashine ambayo inazalisha dawa za nyuklia (radioisotopes) ambazo mgonjwa atapatiwa.
Mkurugenzi Mtendaji Dkt Julius Mwaiselage (aliesimama) akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Mradi
Baada ya wasilisho la taarifa ya utekelezaji, kamati ya bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii, ilifanya ziara kutembelea Kutembelea Taasisi na hasahasa kuangalia eneo lililotengwa kwa ajili ya Mradi wa PET/CT scan, kuangalia Huduma za Tiba Mionzi za LINAC na kuangalia Huduma za Nuclear Medicine.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii kwa niba ya wajumbe, aliipongeza sana Serikali ya awamu ya tano na Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa uwekezaji na utekelezaji makini uliozingatia sheria za manunuzi na mikataba. Mwenyekiti alisema kuwa uwekezaji huo wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha kufanya vipimo vya Saratani kwa kutumia PET Scan na ujenzi wa kiwanda cha kuzalishia mionzi dawa ya radio isotopes itaifanya nchi ya Tanzania kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa kimatibabu.
Akielezea kuhusiana na mradi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima alisema, “Serikali inafanya mapinduzi makubwa na makini katika kuhakikisha kuwa ubora wa huduma za afya kwa watu wote zinaimarishwa na kutolewa kwa wakati na ufanisi. Na kwa kuwa magonjwa yasiyoambukiza yana njia za kuzuia ikiwamo kufanya mazoezi, basi amewashajihisha watanzania kujua njia za kujikinga na kufanya mazoezi kwa wingi.