WAZIRI WA AFYA, MHE. UMMY MWALIMU AMEAGIZA TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD (ORIC) KUANZA KUTOA MATIBABU YA PET -CT SCAN

      Comments Off on

WAZIRI WA AFYA, MHE. UMMY MWALIMU AMEAGIZA TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD (ORIC) KUANZA KUTOA MATIBABU YA PET -CT SCAN

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORIC) kuanza kutoa matibabu ya PET -CT Scan ifikapo Februari Mosi Mwaka huu, kutokana na kukamilisha kwa jengo la kutoa huduma hiyo na kufungiwa mashine hiyo ya mionzi, kwani sababu kubwa ya wagonjwa wengi wa saratani kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Waziri Ummy aliyasema hayo mapema leo alipofanya ziara hapa Taasisi ya Saratani Ocean Road na kukagua jengo jipya litalotumika kutoa huduma za mionzi ikiwemo PET CT, pamoja na Cyclotron.

Aidha waziri Ummy Alisema kuwa wataendelea kuboresha huduma zaidi hususan kujenga wodi nzuri zenye ubora, kuhakikisha wanawavutia watu wa viwango tofauti vya maisha kuja kutibiwa nchini.

Waziri Ummy alisema serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika Taasisi hiyo, kuhakikisha inaboresha huduma zake na miundombinu, ili watanzani wapate huduma bora za matibabu ya saratani.

Kuhusu kuanza kwa mashine ya PET CT Scan, aliwataka kuhakikisha wanaanza huduma hizo za matibabu haraka kutokana na kukamilika miundombinu ya kutolea huduma, ambapo atawaomba kiongozi mmoja kuizindua ili kuanza rasmi kutoa huduma kwani ndio sababu kubwa ya wagonjwa hao kwenda nje ya nchi.

Katika hatua nyingine waziri Ummy aliagiza ORCI, kuhakikisha wanaanza kutoa huduma za upasuaji wa saratani ili kuwaepushia usumbufu wagonjwa kuzunguka katika hospitali zingine, wakati wangependa kutibiwa hospitalini hapo na kumaliza kila kitu.

“Mmenambia kila kitu mnacho, chumba kipo mtaalamu mnaye, hivyo hadi kufika Julai Mosi, muwe mmeanza kutoa huduma hii, mana hiyo itakuwa inaakisi dhamira nzima ya Taasisi hii ya saratani na umahiri wake wa kuwa kituo bora cha umahiri wa kutibu saratani na kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali hususani katika mashine za mionzi,” alisema

Alisisitiza kuwa, serikali itaendelea kusikiliza Taasisi hiyo katika kuwajengea uwezo hivyo na wao wahakikishe wanatanua utoaji wa huduma na kuwajengea uwezo wataalamu katika hospitali za Kanda na mikoa.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy, ameipongeza Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa utoaji huduma bora zilizopunguza malalamiko kwa wananchi na kusaidia Watanzania wengi kupitia huduma zinazopatikana katika hospitalini hapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Julius Mwaiselage alimshukuru Waziri Ummy kufanya ziara katika taasisi hiyo huku akimpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea fedha za ujenzi wa miundombinu.

Alisema kwasasa wanayo mipango mbalimbali ya kujenga jengo jipya katika eneo la tasisi hiyo, huku wakiendelea na mipango ya kuandaa michoro ya ujenzi wa majengo ya kutoa matibabu ya saratani Dodoma na Mbeya.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dk.Mark Mseti alisema wataendelea kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi ikiwemo kutoa msamaha kwa wagonjwa wasio na uwezo.

TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD LEO IMEPOKEA MSAADA WENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 137 KUTOKA KWA KAMPUNI YA GSM

      Comments Off on

TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD LEO IMEPOKEA MSAADA WENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 137 KUTOKA KWA KAMPUNI YA GSM

Taasisi ya Saratani Ocean Road leo imepokea msaada wenye thamani ya Shilingi milioni 137 kutoka kwa mmiliki wa kampuni za GSM Bw. Ghalib Said Mohamed katika kusheherekea siku yake ya kuzaliwa, ambapo pamoja na msaada huo ameshiriki chakula na watumishi wa Taasisi hiyo pamoja na wagonjwa.

Katika sherehe hiyo ambayo imefanyika katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Albert Chalamila ndiye alikuwa mgeni rasmi ambapo ametoa wito kwa watanzania kutoa sadaka ili kuwasaidia wagonjwa katika mahitaji yao ya matibabu kama ambavyo amefanya leo Bw. Gharib Mohamed.

Aidha Mh. Chalamila amesema kuwa watanzania hatuna budi kumshukuru Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mashine mbalimbali katika Taasisi hii ikiwemo Pet CT-Scan ambayo itaweza kuchunguza Saratani katika hatua ambazo mashine nyingine hazitaweza huku akisisitiza kuwa muda si mrefu itaanza kufanya kazi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage amemshukuru mmiliki wa GSM kwa msaada wake aliotoa wa vifaa hivyo.

Dkt. Mwaiselage amesema vifaa hivyo ikiwemo vile vya Tiba ya Saratani vitasaidia katika huduma mbalimbali kwa wagonjwa wa Taasisi hiyo, huku vikirahisisha utoaji wa huduma hizo kwa jamii ya watanzania na wanaotoka nje ya mipaka ya Tanzania.

MAADHIMISHO YA WIKI YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZWA

      Comments Off on

MAADHIMISHO YA WIKI YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZWA

Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akimsikiliza mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage akizungumza kuhusu huduma zinazotolewa hapa Mnazi mmoja katika banda la Taasisi hiyo.

Leo ndio maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukizwa ambapo Taasisi ya Saratani Ocean Road ipo hapa Mnazi Mmoja ikitoa huduma za uchunguzi wa Saratani za Matiti, Mlango wa kizazi pamoja na Tezi dume bila malipo yoyote, hivyo watu wote wanakaribishwa kufanya uchunguzi huu.

Dkt. Mollel ndie mgeni rasmi wa maadhimisho hayo yanayofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja ambapo amekuja kumuwakilisha waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa kassim Majaliwa.

TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD MAPEMA LEO IMEPOKEA TUZO YA HESHIMA YA KUTAMBUA MCHANGO WAKE KATIKA KUONA NAMNA GANI IMESHIRIKI KWENYE KUTOA ELIMU…

      Comments Off on

TAASISI YA SARATANI OCEAN ROAD MAPEMA LEO IMEPOKEA TUZO YA HESHIMA YA KUTAMBUA MCHANGO WAKE KATIKA KUONA NAMNA GANI IMESHIRIKI KWENYE KUTOA ELIMU…

Taasisi ya Saratani Ocean Road mapema leo imepokea tuzo ya heshima ya kutambua mchango wake katika kuona namna gani imeshiriki kwenye kutoa elimu, kufanya uchunguzi pamoja na matibabu ya magonjwa hayo.

Tuzo hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof. Paschal Rugajo wakati wa mkutano wa kimataifa wa kisayansi wa magonjwa yasiyoambukiza unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere.

Akizungumza wakati wa maonesho hayo leo mchana, Prof. Rugajo amesema kuwa katika kipindi hiki Taasisi ya Saratani Ocean Road imekuwa ikifanya vizuri sana kwenye utoaji wa tiba na hii imepelekea kuaminika na mataifa ya jirani na kupelekea kupata wateja wengi kutoka nje wakihitaji kuja kutibiwa hapa katika Taasisi hiyo.

Akisisitiza Prof. Rugajo
Amesema utoaji wa huduma bora ni chachu kubwa ya tiba utalii, na ndio kitu pekee ambacho kwa sasa Tanzania inaendelea kukitilia mkazo ili kuweza kupata matokeo chanya hususan kwenye sekta hii ya Afya.

Maonesho haya yatafanyika kuanzia leo tarehe 01/11/2023 mpaka siku ya Ijumaa tarehe 03/11/2023 katika kukuza ufahamu juu ya magonjwa haya yasiyoambukizwa kwa wananchi.

UCHUNGUZI WA MAPEMA WA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI PAMOJA NA CHANJO YA PAPILLOMA VIRUS ITASAIDIA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI

      Comments Off on

UCHUNGUZI WA MAPEMA WA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI PAMOJA NA CHANJO YA PAPILLOMA VIRUS ITASAIDIA KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI

“Uchunguzi wa mapema wa Saratani ya mlango wa kizazi pamoja na chanjo ya papilloma virus itasaidia katika mapambano dhidi ya Saratani ya mlango wa kizazi”.

Hayo yamesemwa na mtaalamu kutoka University of Calfornia, San Diego Dkt. Chiku Nwachukwu leo wakati anawasilisha mada inayozungumzia mionzi Tiba ya ndani kwa njia ya kisasa kwa Saratani ya mlango wa kizazi ( 3D Brachytherapy In Cervical Cancer).

Dkt. Nwachukwu amefafanua namna njia hiyo ya kisasa inavyoweza kuleta matokeo Bora zaidi katika matibabu hayo ya Saratani ya mlango wa kizazi.

Kwa upande wa waliohudhuria katika mafunzo hayo, wamepata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusiana na tiba hiyo ya kitaalam ambapo kila mmoja slipata majibu kutoka kwa wataalam mbalimbali wa tiba hiyo waliojitokeza.

Ikumbukwe kuwa Taasisi ya Saratani Ocean Road imekwisha anza kutoa huduma ya mionzi tiba ya ndani kwa njia ya kisasa kuanzia mnamo mwezi wa Tano mwaka 2023.

KILELE CHA MKUTANO WA KIMATAIFA WA KISAYANSI WA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA JULIUS NYERERE DAR ES SALAAM

      Comments Off on

KILELE CHA MKUTANO WA KIMATAIFA WA KISAYANSI WA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA JULIUS NYERERE DAR ES SALAAM

Leo ikiwa ni kilele Cha mkutano wa kimataifa wa kisayansi wa magonjwa yasiyoambukiza katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere Dar es Salaam.

Katika mkutano huo madaktari kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road nao wamepata nafasi ya kuwasilisha mada zao.

Madaktari hao Ni Dkt. Harrieth Noah, Dkt. Felister Tupa na Dkt. Goodfrey Malangwa.

Pia wakati huo huo wa mikutano Banda la Taasisi ya Saratani Ocean Road limekuwa likitoa Elimu kuhusiana na Saratani.

Aidha ikumbukwe kuwa Taasisi ya Saratani Ocean Road hivi karibuni imepokea tuzo ya heshima ya kutambulika mchango wake katika kutoa elimu, kufanya uchunguzi na matibabu ya Saratani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt.Julius Mwaiselage leo amepokea msaada wa millioni arobaini kutoka Bodi ya michezo ya kubahatisha Tanzania (GBT).

      Comments Off on

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt.Julius Mwaiselage leo amepokea msaada wa millioni arobaini kutoka Bodi ya michezo ya kubahatisha Tanzania (GBT).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt.Julius Mwaiselage leo amepokea msaada wa millioni arobaini kutoka Bodi ya michezo ya kubahatisha Tanzania (GBT).

Bodi ya michezo ya kubahatisha Tanzania (GBT) imetoa msaada huo katika kuadhimisha miaka ishirini ya Bodi hiyo ya michezo ya kubahatisha Tanzania.

Bodi hiyo imetoa bedside Mia moja zenye thamani ya Shilingi milioni ishirini na nne, Hundi yenye thamani ya Shilingi milioni kumi na tano pamoja na vifaa mbalimbali ikiwemo sabuni na maji.

Akitoa shukrani zake Dkt. Mwaiselage amesema msaada huo utakwenda kuimarisha maeneo ya ugonjwa, pamoja na kwa wagonjwa moja kwa moja.

Pia Dkt. Mwaiselage ameahidi msaada huo utakwenda pale ulipokusudiwa kwa Usimamizi madhubuti huku akitoa wito kwa wadau wengine kuleta misaada zaidi na milango ya Taasisi ipo wazi kupokea misaada mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya kubahatisha Tanzania (GBT) Bw. James Mbalwe amesema katika kusaidia Jamii ni Jambo la lazima sio hiari, ndio mana wao wameamua kurudisha kile kidogo walichopata kwa jamii.

Bw. Mbalwe ameongeza kuwa kujitolea kwa kutoa misaada kwa pamoja italeta tija kubwa kwa Jamii inayotuzunguka.

Aidha Bodi hiyo ya Michezo ya kubahatisha Tanzania (GBT) imeambatana na wadau wa michezo hiyo ya kubahatisha nchini katika kutoa misaada hiyo.

AFISA MIRADI WA SHIRIKA LA KIMATAIFA LA NGUVU ZA ATOMIC BI.AZA KASHLAN AMESEMA

      Comments Off on AFISA MIRADI WA SHIRIKA LA KIMATAIFA LA NGUVU ZA ATOMIC BI.AZA KASHLAN AMESEMA

Afisa miradi wa shirika la kimataifa la nguvu za Atomic Bi.Aza Kashlan amesema kuwa pamoja na msaada wa mashine walizozitoa kipindi cha nyuma, ila bado wataendelea na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo mashine kwa namna itakavyowezekana ili kurahisisha matibabu katika Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Bi. Kashlan amesema mapema mwakani kutakuwa na mradi mwingine mkubwa ambao wanategemea pindi ukikamilika watauleta hapa katika Taasisi hii.

Akizungumza katika majadiliano maalum yaliyofanyika katika ukumbi uliopo ofisini kwake, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt Julius Mwaiselage amesema kuwa ujio wa kiongozi huyu umempa nafasi ya kuzungumza nae mambo mbalimbali ikiwamo, kuanzisha shahada ya uzamili kwenye fizikia tiba, ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kitabibu mfano, mashine za tiba n.k pqmoja na mafunzo upande wa uchunguzi kwenye mambo ya CT Scan.

Bi. Kashlan ameahidi kuitekeleza miradi yote ambayo Dkt. Mwaiselage amemuomba pindi tu muda utakapofikia kwa kuanzia na mambo kadhaa mapema mwakani.

TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD IMEANZA KUTOA HUDUMA YA MIONZI TIBA YA NDANI KWA NJIA YA KISASA (3D INTRACAVITARY BRACHYTHERAPY)

      Comments Off on

TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD IMEANZA KUTOA HUDUMA YA MIONZI TIBA YA NDANI KWA NJIA YA KISASA (3D INTRACAVITARY BRACHYTHERAPY)

Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imeanza kutoa huduma ya mionzi tiba ya ndani kwa njia ya kisasa (3D INTRACAVITARY BRACHYTHERAPY) kwa wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.

Hayo yamesemwa wiki hili na Dkt Faraja Kiwanga ambaye ni daktari bingwa wa saratani kutoka kliniki ya Bima (HIC) alipokuwa akiwasilisha maada na kuitambulisha huduma hiyo ambayo imeanza kutolewa katika Taasisi kuanzia mnamo mwezi wa tano mwaka huu 2023.

Huduma hii ni ya kibingwa bobezi ambayo inatumia vifaa vya kisasa kuanzia kwenye kumuandaa mgonjwa, kumuwekea vifaa tiba kwa ajili ya mionzi, kutumia kipimo cha CT scan kuangalia kama vifaa tiba vimekaa mahali pake vizuri, pia kutumia picha za CT scan kufanya kontua kwenye sehemu ambapo ugonjwa upo na kufanya kontua kwenye ogani zinazokaribia eneo linalotakiwa kupata tiba ya kutosha na bila kuathiri ogani zilizokaribu, pia kutumia picha za CT scan kupanga tiba na kufanya mahesabu ya dozi ya mionzi tiba na kuhakikisha kuwa ugonjwa unatibiwa kwa ubora wa hali ya juu.

Akichangia maada hiyo Kaimu Mkuu wa Kliniki ya Bima, Dkt Emmanuel Lugina alisema, huduma hii ni muhimu sana hasa ikizingatia kuwa saratani ya mlango wa kizazi ni Saratani inayoongoza kwa idadi ya wagonjwa, hivyo wahudumu wa afya wanapowaona wagonjwa wajikite katika kuwafanyia uchunguzi (clinical examination) na pia kuweka kumbukumbu (documentation) ili kuweza kupanga aina ya mionzi tiba ambayo itamfaa mgonjwa na pia katika kuongeza tafiti katika eneo hili.

Naye Dkt Nuru Mlagalila alichangia kuwa huduma hii ya mionzi tiba ni muhimu kwa wagonjwa wetu wanaotufikia katika taasisi kwa kuwa wengi wa wagonjwa wanafika katika hatua ya pili na ya tatu, ambapo wakipata huduma hii watapata matokeo mazuri ya tiba.

Huduma hii inatolewa kwa ushirikiano wa daktari bingwa wa saratani (clinical Oncologist), Mfizikia Tiba (Medical Physicist), mtaalamu wa mionzi tiba (Radiation Therapist), na wauguzi (Brachytherapy Nurse).

Huduma hii inapatikana katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Block C kwenye chumba cha Mionzi ya Ndani kila siku kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa kumi na moja jioni Jumatatu hadi Ijumaa.

Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo ametembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road

      Comments Off on

Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo ametembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road

Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo ametembelea Taasisi ya Saratani Ocean Road na kuzungumza na baadhi ya watumishi, huku akiupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kusimamia vizuri pesa zinazotolewa na serikali kwaajili ya miradi mbalimbali.

Dkt. Mollel amesisitiza kuwa ujenzi wa jengo mfano la Cyclotron ukiliangalia kwa nje unaweza Sema limegharimu kiasi kidogo sana cha pesa ila kwa ndani ndio utagundua thamani ya pesa iliyotumika kuwa inaendana na ubora na umadhubuti wa jengo lenyewe.

Dkt. Mollel ameomba uharaka wa umaliziaji wa jengo hilo ufanyike kwani watanzania wanahitaji huduma zake mapema iwezekanavyo huku serikali ikitaka uwekezaji wake uanze kuleta tija kwa wananchi.

Nae mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt Julius Mwaiselage, amemhakikishia Dkt. Mollel kumalizika mapema kwa ujenzi huo kwani kwa upande wa jengo limekamilika kwa Asilimia tisini na nane wakati mashine tayari zimekwishasimikwa kwa asilimia Mia moja huku ukisubiriwa utaratibu wa kuunganisha umeme pekee ili mashine hizo zianze kutumika kama inavyotakiwa.

Jengo hilo limekusanya mashine mbili kubwa ambazo ni PET-CT SCAN pamoja na CYCLOTRON (kiwanda cha kutengeneza mionzi) ambapo kwa sasa kwa Tanzania nzima kitakuwa ni kimoja tu, ambacho kitakuwa kikitengeneza mionzi ambayo itatumika kwa Taasisi huku mingine ikipelekwa kwenye hospitali nyingine kwaajili ya kusaidia wahanga wa huko. Kwa sasa Taasisi inanunua mionzi hiyo kutoka Afrika ya Kusini huku gharama zake zikiwa kubwa mno ukilinganisha na uwezo wa watanzania wenyewe, hivyo kukamilika kwa usimikaji huo kutakuwa msaada mkubwa sana kwa Tanzania na Afrika mashariki na kati kwa ujumla.