Uzinduzi wa Muongozo wa Tiba ya Saratani nchini Tanzania na Tamko la Waziri afya katika Siku ya Saratani Duniani

      Comments Off on Uzinduzi wa Muongozo wa Tiba ya Saratani nchini Tanzania na Tamko la Waziri afya katika Siku ya Saratani Duniani

Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb) mnamo tarehe 03/02/2019 katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road , akiwa ni mgeni rasmi, alizindua rasmi muongozo wa taifa wa tiba ya saratani na kutumia fursa hiyo kutoa tamko la Serikali katika maadhimisho ya siku ya Saratani duniani yanayofanyika Tarehe 4 Februari ya kila mwaka. Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alieleza kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Mimi na Nitafanya”.

Pia, alishajihisha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kuendeleza na kutoa elimu za visababishi, dalili za kutambua saratani na kile kinachopaswa kufanyika pale ambapo tayari Mwananchi anapokuwa amegundulika na ugonjwa wa Saratani. Aliitaka Taasisi ya Saratani Kuendelea kutoa mtazamo chanya na kujikita Zaidi katika kutoa huduma bora kama zinavyoelekezwa katika muongozo unaozinduliwa.

Waziri Ummy Mwalimu alizindua muongozo huo na kutoa takwimu za ukubwa wa tatizo la saratani duniani na hapa nchini, huku akipongeza juhudi zilizopo nchini Tanzania za kuongeza hospitali za kutibu wananchi dhidi ya ugonjwa wa Saratani. Takwimu zinaonyesha kuwa katika kila watu 100,000 kuna wagonjwa 76 wapya wa saratani. Huku vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo kufikia 68 kwa kila wagonjwa 100. Hali hii ya vifo inatokana hasa na wagonjwa wengi kuhudhuria hospitali wakiwa katika steji ya mwisho.

Waziri Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Muongozo wa Taifa katika kutoa tiba ya Saratani

Waziri aliwashukuru wadau walioshiriki katika kufanikisha kuandaa mpango huo wa taifa wa tiba ya saratani na kuwataka wanahabari kubeba jukumu la kuelimisha wananchi, ili kuongeza idadi ya wananchi wanaoenda hospitali kufanya uchunguzi na hivyo kugundua tatizo mapema na kuongeza idadi ya wanaotibiwa na kupona.

Waziri Ummy aligawa nakala za muongoz huo wa Taifa kwa wakurugenzi na wawakilishi wa wakurugenzi wa hospitali zinazotoa matibabu ya ugobjwa wa saratani nchini ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, MOI, Bugando na KCMC. Pia aligawa nakala za vyeti vya shukrani kwa wadau waliochangia kufanyika kwa kazi ya kuandaa muongozo huo wa kitaifa. Wadau hao ni Pamoja na American Cancer Society, Roche pharmaceutical Tanzania, HeteroBiopharama LTD na University of California San Fransisco,

Waziri Ummy Mwalimu akimkabidhi cheti cha shukran mwakilishi wa University of California San Fransisco

Awali Akimkaribisha mgeni rasmi, kuhutubia na kuzindua muongozo huo wa taifa, Dr Grace Maghembe alimueleza Mheshimiwa Waziri kuwa Saratani bado ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza duniani kwa kusababisha vifo kwa watu wengi. Dr Maghembe alieleza kuwa, kutokana na takwimu hizo, na kwa kuwa tayari huduma za kutibu ugonjwa wa Saratani nchini Tanzania zimeongezeka kwa hospitali nyingi Zaidi kutoa huduma hizo, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na wadau wengine wa afya, waliandaa timu ya Pamoja ya kuandaa mpango wa taifa wa kusimamia utoaji wa huduma za Saratani.

Dr Maghembe alisema kuwa muongozo huo unatoa maelekezo na majukumu ya kila ngazi ya hospitali kutoka zahanati mpaka kufikia hospitali bingwa na za rufaa. Kwa kiasi kikubwa, muongozo umezingatia sana kinga, kwani kinga ni bora kuliko tiba. Hivyo uchunguzi wa mapema wa kila aina ya saratani umezingatiwa na umeelezwa kwa kina katika muongozo huo.

Nae, Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, alieleza kwa kina namna ambavyo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imejiimarisha na kuboresha huduma zake kuanzia 2015. Mkurugenzi huyo alieleza kazi kubwa iliyofanywa na wafanyakazi wa Ocean Road na timu iliyoteuliwa katika kuandaa muongozo huo na kuwanasihi sana wataalamu wa hospitali zote zinazotoa matibabuu ya saratani nchini kuzingatia kwa kina yaliyoelezwa kwenye muongozo huo. Pia alitumia fursa hiyo, kuwaeleza wananchi kwa ujumla kuwa, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road katika wiki hii ya maadhimisho ya Ugonjwa wa Saratani duniani, kuwa itaendelea na kutekeleza majukumu yake ya kufanya zoezi la uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani.

Mkurugenzi aliwashukuru sana, wadau wote walioshirikiana na Wizara ya Afya na Taasisi ya Ocean Road katika kuandaa muongozo huo.